EACC yanasa polisi wa trafiki na mabunda ya pesa za hongo
TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Desemba 30, 2025, iliwakamata maafisa wawili wa polisi wa trafiki katika miji ya Murang’a na Mtwapa kwa madai ya kuomba na kupokea hongo kutoka kwa madereva barabarani.
Huko Murang’a, EACC ilimkamata afisa wa cheo cha konstebo Kelvin Mwangi anayehudumu katika Kituo cha Trafiki cha Murang’a, kufuatia operesheni maalum ya ufuatiliaji katika barabara yenye shughuli nyingi ya Kenol–Murang’a. Tume ilisema kwamba operesheni hiyo ilianzishwa baada ya kupokea malalamishi kadhaa kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vya hongo vya maafisa wa trafiki katika eneo hilo.
Baada ya upekuzi, maafisa wa EACC walipata Sh6,450 katika noti za Sh50, Sh100 na Sh200, fedha zinazodhaniwa kukusanywa ndani ya kipindi cha saa mbili. Afisa mwingine wa cheo cha konstebo alihepa kukamatwa.
Mshukiwa alipelekwa hadi ofisi za EACC Kanda ya Kati kwa taratibu za kisheria, kisha akafikishwa katika Kituo cha Polisi cha Nyeri ambako aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu akisubiri kukamilika kwa uchunguzi.
Katika operesheni hiyo hiyo, maafisa wa EACC walivamia eneo lingine linalodhaniwa kutumika kukusanya hongo katika barabara ya Kerugoya–Kutus karibu na eneo la Bekam, ambapo maafisa wa trafiki walitoroka na kujificha vichakani, wakiacha nyuma sare rasmi za polisi.
Katika operesheni tofauti katika Pwani, maafisa wa EACC walimkamata Koplo wa Polisi Haroun Mazera Chamutu, anayehudumu katika Kituo cha Trafiki cha Mtwapa, kwa tuhuma za kuomba hongo kutoka kwa madereva katika barabara kuu ya Mombasa–Malindi. Wakati wa kukamatwa alipatikana na Sh13,750 kwa noti mbalimbali. Alipelekwa hadi ofisi za EACC mjini Malindi kurekodi taarifa na hatua zaidi za uchunguzi.
EACC ilisema operesheni hizi ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kitaifa za Tume kupambana na ufisadi katika barabara kuu, hasa katika msimu wa sherehe.
“EACC inaendelea kuimarisha ukusanyaji wa taarifa za kijasusi na ufuatiliaji katika huduma muhimu za umma na sekta zilizo katika hatari ya ufisadi, kwa lengo la kuhimiza uadilifu, uwajibikaji na taaluma katika utumishi wa umma,” tume ilisema kwenye taarifa.
Tume inawahimiza wananchi kuendelea kuripoti vitendo vya hongo kupitia njia rasmi za kuripoti za EACC.