Habari

Bidhaa kuu za magendo Kenya ni sukari na pombe, ripoti yabaini

December 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SUKARI, pombe na sigara zilichangia sehemu kubwa ya bidhaa haramu na bandia zilizonaswa na maafisa wa usalama kufikia Agosti 2025.

Ripoti ya serikali inaonyesha kuwa bidhaa haramu zilizosafirishwa kwa wingi ni pamoja na sukari, vifaa vya kielektroniki, sigara, pombe, dawa na vipodozi.

Ripoti ya Mwaka ya Hali ya Usalama wa Taifa inayohusu kipindi cha Septemba 1, 2024 hadi Agosti 2025, pia inaonyesha matumizi ya vifaa na apu haramu za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).

Ripoti hiyo, iliyowasilishwa Bungeni na Rais William Ruto, inaonyesha kuwa maafisa wa usalama walinasa kilo 52,075 za sukari, lita 24,570 za pombe, pakiti 9,707 za sigara, katoni 24,570 za mvinyo pamoja na bidhaa nyinginezo.

Bidhaa nyingine zilizonaswa na polisi ni pamoja na lita 338 za mafuta ya kupikia, kiasi hiki kikipungua kutoka lita 879 zilizonaswa katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

Magunia ya mbolea haramu yaliyonaswa yalikuwa 685 ikilinganishwa na 521 katika kipindi sawa mwaka uliotangulia, huku maziwa yaliyoingizwa nchini kinyume cha sheria yakiongezeka kutoka lita 2,390 hadi lita 3,437.

Cha kushangaza, hakuna mchele haramu au bandia ulionaswa katika kipindi hicho ikilinganishwa na tani 19,900 za mchele zilizonaswa mwaka mmoja kufikia Agosti 2024.