AG, LSK sasa waingizwa ndani ya kesi ya refarenda
MAHAKAMA Kuu ya Milimani imewajumuisha Mwanasheria Mkuu (AG) Dorcus Oduor, Katiba Institute na Chama cha Wanasheria nchini (LSK) katika kesi ambapo korti inaombwa izuie Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kusimamia Kura ya Maoni (refarenda) na Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Kesi hiyo inashutumu IEBC kwa kutotathmini upya majina ya maeneo ya uwakilishi bungeni na wadi.
Huku akiagiza AG, LSK na Katiba Institute wawasilishe ushahidi ama wa kupinga au kuiunga mkono kesi hiyo, Jaji Bahati Mwamuye alisema kesi hii imezua masuala nyeti na yenye umuhimu mkubwa kwa umma.
Jaji Mwamuye aliamuru pande zote ziwasilishe ushahidi kortini kufikia kesho Januari 2, 2026
Kesi ya kuzima IEBC kusimamia kura ya maoni (refarenda) iliyopendekezwa na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Uchaguzi Mkuu 2027 iliwasilishwa kortini na Bw Philip Kipkempoi Langat mnamo Desemba 22, 2025.
Baada ya kutathmini masuala aliyozua katika kesi hiyo, Jaji Mwamuye aliamua kushirikisha AG, LSK na Katiba Institute watoe mchango wao kujibu masuala saba aliyozua Bw Langat.
Katika kesi hiyo, Bw Langat amedai kwamba IEBC katika muda wa miaka 12 iliyopita haijawahi kutathmini upya majina ya maeneo ya uwakilishi bungeni, kuongeza idadi ya maeneo ya uwakilishi bungeni na wadi.
Mahakama imeelezwa kwa mujibu wa Kifungu nambari 89 (2)(3) cha Katiba, IEBC inatakiwa kutathmini upya majina ya maeneo ya uwakilishi bungeni pamoja na wadi mbali na kuongeza idadi ya maeneo ya bunge.
Kwa mujibu wa vipengee hivi, zoezi hilo linatakiwa kutekelezwa katika muda wa miaka minane (8) na kumi na miwili (12).
“Kila utathmini upya wa maeneo ya uwakilishi bungeni na wadi unatakiwa kufanywa miezi 12 kabla ya uchaguzi mkuu wa wabunge,” asema wakili Felix Keaton aliyewasilisha kesi hiyo kwa mujibu wa sheria za dharura.
Hata hivyo, mahakama ilikataa kuzima IEBC kutosimamia kura ya maoni au uchaguzi mkuu wa 2027 na badala yake iliagiza kesi hiyo ipewe kipau mbele.
Hata hivyo, mlalamishi (Philip Kipkemoi Langat) amesema kwamba zoezi hilo halingefanyika Machi 6, 2024 kwa vile hakukua na tume ya uchaguzi kufuatia kujiuzulu kwa makamishna watatu baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2022
Na wakati huo huo, tume ya IEBC iliyoongozwa na marehemu mwenyekiti Wafula Chebukati ilipata pigo nyingine baada ya kamishna mmoja kutimuliwa na jopo na makamishna wengine watatu wakastaafu baada ya muda wao wa kuhudumu kuyoyoma.
Lakini sasa Bw Langat amesema IEBC iko na makamishna wote baada ya kuteuliwa na Rais William Ruto Juni 10, 2025.
Mlalamishi huyo amesema IEBC inatakiwa kuendeleza zoezi hilo la kutaja maeneo mapya ya uwakilishi bungeni kwa vile imekamilika kufuatia uteuzi wa Erastus Edung Ethekon na makamishna wengine na Rais Ruto.
Mnamo Juni 10, 2025 Rais Ruto aliwateua makamishna sita wapya wa IEBC miongoni mwao aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Njeri Nderitu.
Makamishna wengine ni Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol na Fahima Araphat Abdallah.
“Baada ya kuteuliwa tume hii imekataa kutekeleza majukumu yake ya kutathmini upya mipaka kwa mujibu wa sheria,”mlalamishi huyu amedai.
Mara ya mwisho IEBC ilitekeleza jukumu hilo la kutathmini upya mipaka ni Machi 6, 2012
IEBC ilitakiwa kuendeleza zoezi hilo Machi 6, 2020 ikiwa ni miaka minane kwa mujibu wa sheria.
Kufikia Machi 6, 2024 ilikuwa ni miaka 12.
Malalamishi anaomba mahakama kuu itumie mamlaka iliyopewa kwa mujibu wa Kifungu nambari 165 (2)(d) kutafsiri baadhi ya vipengee vya katiba kuhusu zoezi hili.
Mahakama imeombwa itoe mwelekeo ikiwa kuna athari zozote utathmini huu wa mipaka, majina ya maeneo na wadi na uzinduliwaji wa maeneo mapya kutofanywa.
Mahakama imeamuru kesi hiyo isikizwe Januari 28, 2026.