Maoni

MAONI: Tunapoanza mwaka huu mpya, tujiwekee maazimio yanayojikita katika uhalisia

January 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 1

SALAMU za Mwaka Mpya! Iwapo unasoma makala haya, hiyo ni ithibati tosha kwamba, licha ya pandashuka na mihemko ya 2025, Maulana amekujaalia kuvuka salama na kuiona 2026.

Ilipotimia saa sita kamili usiku wa kuamkia leo, kuna malengo, maamuzi na shauku la moyo wako ambalo, kama wewe ni muumini, ulimnong’onezea Mola kuwa ungependa kufanikisha Mwaka Mpya na hata kunakili sehemu fulani kama ukumbusho.

Mwaka Mpya huja na matumaini kuhusu mwanzo mpya. Ni wakati muhimu wa kusahau yaliyopita na kufungua ukurasa mpya kama mtu binafsi, wanandoa, familia, jamii na taifa kwa jumla.

Kuweka maazimio ya Mwaka Mpya au kutoyaweka, ni mdahalo mzima kivyake. Kila mtu ana mambo anayotamani kufanikisha, kubadilisha au viwango anavyokusudia kufikia maishani.

Huenda maazimio yako ya Mwaka Mpya yanajumuisha kuwa na muda zaidi na familia na wapendwa wako, kujitunza kiafya, kuacha matumizi ya mihadarati, kukatiza mahusiano hasi, kuweka akiba, kujiimarisha kifedha, kulipa madeni, kujituma zaidi kazini au shuleni, kufungua biashara na mengineyo.

Hata hivyo, ni sharti maazimio ya Mwaka Mpya tunayopanga yawe ya uhalisia na yajumuishe mikakati kabambe kuhusu jinsi ya kuyafanikisha, tukifahamu fika kwamba kufeli kupanga ni kupanga kufeli.

Tunapoanza Mwaka Mpya, ni muhimu zaidi kuepuka jaribio la kujilinganisha na wenzako uliolelewa au kusoma nao ambao sasa unahisi wamepiga hatua zaidi maishani na kukuacha nyuma iwe kielimu, kitaaluma, ndoa, na kadhalika.

Anza mwaka wa 2026 na moyo uliofurika shukran na matumaini ukikumbuka kwamba maisha ni safari na kila binadamu ana hatima yake ya kipekee aliyojaliwa na Mola.