Afya na Jamii

Manufaa na madhara ya kuvalia soksi wakati wa kulala

Na WANGU KANURI January 2nd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KUNA watu duniani ambao wanapolala wakiwa wamevaa soksi hupata usingizi mwanana, huku wengine wakishindwa kabisa kulala wakiwa wamezivaa.

Mtaalam wa masuala ya usingizi, Mwende Kimweli, anasema kuwa kwa watu wengi, kulala na soksi husaidia kupata usingizi.

Miguu yenye joto hutuma ujumbe kwa ubongo kwamba ‘unaweza kupumzika’ jambo linalosaidia mwili kulala haraka.

“Miguu baridi hufanya kinyume chake. Huifanya mishipa ya damu kujikaza na kuuweka mwili tayari kwa hivyo, Wakenya wanaoishi katika maeneo ya Limuru, Nyeri au Eldoret, soksi zinaweza kuwa msaada mkubwa.”

Zaidi ya hayo, kadri muda wa kulala unavyokaribia, mwili hutulia. Joto la ndani ya mwili hushuka, huku mishipa ya damu kwenye mikono na miguu ikitanuka ili kutoa joto.

Kupoa huku, Bi Kimweli anasema ni kichocheo muhimu kinachouambia ubongo, ‘Ni wakati wa kulala.’ Miguu ikiwa baridi sana, mishipa hiyo hujikusanya, na kuchelewesha mwili kutulia.

Hata hivyo, ikiwa unahisi joto au baridi kupita kiasi, mwili huendelea kujitahidi kurekebisha hali hiyo, huku usingizi ukiwa mwepesi au mtu akawa anaamkaamka sana.

Wanaonufaika wanapolala wakiwa wamevaa soksi

Kwa mujibu wa Bi Kimweli, wanaoweza kunufaika zaidi kwa kuvaa soksi wanapolala ni pamoja na watu wenye miguu baridi, wenye mzunguko hafifu wa damu, wanaotatizika kulala (insomnia), wazee ambao mzunguko wa damu hupungua kwa njia ya kawaida, na mtu yeyote anayeishi kwenye maeneo ya baridi au nyumba zenye sakafu baridi.

Kuvaa soksi kunaweza kusaidia kupunguza kuamka usiku au kutolala vizuri, kwa sababu miguu yenye joto husaidia kudumisha hali thabiti ya joto au baridi mwilini usiku kucha.

“Mabadiliko ya halijoto ni mojawapo ya sababu kubwa zinazowafanya watu waamke. Soksi husaidia kudhibiti halijoto na kupunguza kugeukageuka kitandani.”

Zaidi ya hayo, Bi Kimweli anasema kuwa kuna hali ambazo kupasha miguu joto usiku kunapendekezwa. Hii ni pamoja na watu wanaougua ugonjwa wa vidole vya mikono au miguu kuwa baridi sana au kufa ganzi unaofahamika kama Raynaud’s, matatizo ya mzunguko wa damu kwenye miguu, hali ya kukosa usingizi inayochochewa na msongo wa mawazo, na kutolala vizuri sababu ya baridi.

Katika hali hizi, Bi Kimweli anasema joto linaweza kuzuia usumbufu unaokatiza usingizi.

Wasiofaa kuvaa soksi wakilala

Hata hivyo, si kila mtu anapaswa kuvaa soksi anapolala. Bi Kimweli anasema watu wanaopaswa kuwa waangalifu au kushauriana na daktari ni pamoja na wenye matatizo sugu ya mzunguko wa damu, na wenye baadhi ya matatizo ya kisukari yanayoathiri miguu.

“Pia, watu wenye maambukizi ya ngozi, vidonda, au ukurutu (eczema) kwenye miguu, na watu wanaotokwa jasho kupita kiasi usiku.”

Hata hivyo, yapo madhara mengine yanaoibuika kwa kulala ukiwa umevaa soksi.

Kwa mfano, soksi zinazobana sana zinaweza kuzuia mtiririko wa damu hasa kwenye vifundo. Hii ni kwa sababu baadhi ya nyuzi zilizotumika kuunda soksi hunasa unyevu na kutengeneza mazingira bora ya fangasi kama fangasi wa mguu (athlete’s foot); na kuvaa soksi chafu ambazo zinaweza washa ngozi au kusambaza bakteria.

Ni soksi gani bora za kulala?

“Unaweza ukachagua soksi laini za pamba, manyoya, mianzi (bamboo), au zile zinazopitisha hewa.

Pia, soksi hizo zinapaswa kuwa huru, zisizobana kifundo cha mguu, na zilizo nyepesi au nzito kulingana na hali ya hewa,” anashauri Bi Kimweli.

Pia, unapaswa kuwa na soksi maalum za wakati wa kulala. Hii ni njia safi zaidi ya kuzuia jasho, uchafu na bakteria. Mbali na soksi, Bi Kimweli anasema unaweza kupasha miguu joto au kudhibiti halijoto ya usiku kwa kuoga maji vuguvugu kabla ya kulala.

“Hii husaidia mwili hutulia baadaye, mtu akalala vizuri,” anaeleza.

Pia unaweza kuweka chupa ya maji ya moto kwenye miguu, kutumia matandiko nyepesi, kuwasha kipasha-joto kwa kiwango cha chini, kuvaa sapatu zenye joto kabla ya kuingia kitandani, au kutia miguu kwenye maji vuguvugu kwa dakika kumi kabla ya kulala.