2026 usiwe mwaka wa ahadi, uwe wa utekelezaji
MWAKA mpya wa 2026 umeanza kwa ahadi nyingi kutoka kwa viongozi wa kisiasa, lakini kama ilivyokuwa kwa miaka mingine, tunahitaji kujiuliza: je, ahadi hizi zitatekelezwa vipi?
Ahadi pekee hazitoshi, utekelezaji ndio unaohitajika ili kuboresha maisha ya Wakenya.
Hii ni hali ambayo imekuwa ikijitokeza kila mwaka, ambapo viongozi wanatoa ahadi nzuri lakini utekelezaji unakuwa wa kutoeleweka au polepole sana.
Ahadi zinazotolewa, kama vile kupunguza umasikini, kupambana na ukosefu wa ajira, na kuboresha sekta za afya na elimu, ni muhimu sana.
Lakini ni muhimu kujiuliza, je, mifumo ya serikali ina nguvu ya kutekeleza mipango hii? Je, kuna mpango mzuri wa kugawa rasilmali kwa usawa ili kuhakikisha kwamba kila raia anafaidika? Haya ni maswali ambayo viongozi wanapaswa kujibu kwa vitendo.
Kwa mfano, ahadi ya kupunguza kiwango cha umaskini na kuongeza ajira inahitaji mikakati ya muda mrefu, kama vile uwekezaji katika viwanda, kilimo, na sekta za huduma.
Hii inahitaji utendaji mzuri wa serikali katika kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inaendeshwa kwa ufanisi, na kwamba fedha za umma zinatumika ipasavyo.
Aidha, kuhakikisha kuwa elimu inafikia kila mtoto nchini, bila kujali hali ya kifamilia, inahitaji uangalizi wa kipekee na utawala bora.
Katika sekta ya afya, ahadi za kuboresha huduma na kuhakikisha upatikanaji wa matibabu bora ni muhimu, lakini utekelezaji wake unategemea sana ufanisi wa mipango ya afya ya jamii, upatikanaji wa dawa, kuajiri wahudumu na wataalamu wa kutosha na usimamizi bora wa rasilmali.
Viongozi wanahitaji kuhakikisha kuwa hospitali zetu zina vifaa vya kutosha, na kuwa watoa huduma za afya wanapata mafunzo bora na malipo ya haki.
Usalama pia ni kipengele muhimu katika utekelezaji wa ahadi hizi. Hakuna maendeleo ya kweli yanaweza kufikiwa katika mazingira ya kutokuwa na usalama.
Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa vikosi vya usalama vinapata mafunzo ya kisasa, vifaa vya kutosha, na usimamizi mzuri ili kukabiliana na vitisho vya uhalifu, ugaidi, na mivutano ya kisiasa.
Viongozi wanapaswa kutoa kipaumbele kwa usalama kama sehemu muhimu ya ustawi wa taifa.
Wakenya wanahitaji kuona matunda ya ahadi hizi, sio tu katika hotuba bali katika vitendo.
Ahadi peke yake hazitoshi, utekelezaji ni muhimu zaidi kuliko maneno. 2026 uwe mwaka wa utekelezaji wa ahadi hizi, na sio tu maneno ya kisiasa.