Wajukuu wa Odinga sasa wasaka nyayo za Raila
Baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kutikisa familia na taifa kwa ujumla, familia ya Odinga imechukua hatua za haraka kulinda na kuhifadhi urithi wa kisiasa.
Badala ya kujitenga na dunia kwa maombolezo, imeendelea kuwa macho kwa mabadiliko ya kisiasa huku azma yao ikiwa ni kuhakikisha ushawishi wa Odinga haukuzikwa pamoja na Raila.
Bila Raila, mzigo mkubwa zaidi wa uongozi, kifamilia na kisiasa, sasa unabebwa na kiongozi wa ODM na Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga. Macho ya taifa yataelekezwa kwake mwaka wa 2026 kufanya maamuzi makubwa, ikiwemo iwapo ODM itasimama kivyake au itaunga mkono muhula wa pili wa Rais William Ruto.
Pia yupo Bi Ida Odinga, mke wa marehemu Waziri Mkuu, ambaye amekuwa akipokea wajumbe katika makazi yake Opoda, Bondo na Karen, Nairobi, huku akitoa matamshi ya kisiasa. Hivi majuzi alisisitiza kuwa ODM lazima imuunge mkono na kumheshimu Dkt Oginga kama kiongozi wa chama katikati ya migogoro inayotikisa chama hicho.
Hata hivyo, kinachozidi kuvuta hisia ni namna kizazi cha tatu cha familia ya Odinga kimejitokeza taratibu kuchukua majukumu. Wajukuu wa Jaramogi wamelazimika kujitokeza na kuandaa mikutano kote nchini kujipanga, si tu ndani ya familia bali pia dhidi ya wagombea wengine wenye nguvu wanaowania uongozi wa jamii ya Luo.
Winnie Odinga, kwa mfano, ni mchanga lakini mwenye ushawishi mkubwa. Alikuwa India pamoja na shangazi yake, Mbunge Mwanamke wa Kisumu Ruth Odinga, wakati Raila Odinga alipofariki. Alirejea nchini akiwa amevaa kofia maarufu ya Panama iliyomtambulisha babake. Tangu wakati huo, ametoa hotuba kali katika mazishi ya babake na maadhimisho ya miaka 20 ya ODM.
Wakati mwingine alionekana kuhoji uwezo wa mjomba wake, Dkt Oginga, kuongoza mazungumzo ya serikali jumuishi, lakini baadaye alitangaza anamtii. “Kiongozi wa chama ni mjomba wangu; nampenda kwa sababu ndiye baba pekee aliyebaki kwangu. Hakuna siku nitakuwa katika mrengo ambao hayumo. Yeye ndiye kichwa cha familia yangu na niko naye daima. Chama chenye wanachama zaidi ya milioni nane lazima kiwe na tofauti za maoni, lakini hilo halimaanishi watu wafurahie kuona ODM ikivunjika,” alisema.
Wapo wanaodai kuwa angekuwa chaguo bora zaidi kama mgombea mwenza wa Rais Ruto mwaka wa 2027.
Kwa upande wake, Raila Odinga Junior ameonekana kuchukua hatamu za familia na amekuwa akijitokeza katika majukwaa mbalimbali ya kisiasa tangu kifo cha babake. Ingawa dada yake amepiga hatua kubwa kisiasa, naye pia anaibuka kama kiongozi mtarajiwa, ingawa amezama zaidi katika masuala ya kibiashara huku akiendelea kutoa maoni kuhusu ODM na masuala ya kitaifa.
Dada yao mkubwa, Rosemary Odinga, anaonekana kujiondoa kidogo katika siasa baada ya kupona ugonjwa uliokaribia kumfanya apoteze uwezo wa kuona. Kabla ya kuugua, alionekana kama mrithi dhahiri wa Odinga baada ya kifo cha ndugu yao Fidel mnamo Januari 4, 2015. Rosemary aliingia kwenye ulingo wa siasa alipotangaza azma ya kugombea kiti cha ubunge Kibra mwaka wa 2017, lakini baadaye alipata kiharusi na kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu. Alijiondoa kwenye kinyang’anyiro baada ya madaktari kumshauri atumikie jamii kwa njia nyingine.
Wana wa Dkt Oginga, Jaoko Oburu na Elijah Oburu, pia wamekuwa wakijihusisha na siasa kwa miaka mingi, ingawa bado hawajachaguliwa. Jaoko aliwahi kuwa Waziri wa Barabara katika Kaunti ya Siaya na hivi majuzi aliteuliwa kuwa Mshauri Maalum wa Rais kuhusu Uwezeshaji wa Kiuchumi na Maisha Endelevu. Amekuwa akifanya mikutano na makundi mbalimbali na kuhudhuria mikutano ya hadhara maeneo ya Kakamega, Pwani na Bonde la Ufa.
Elijah naye alijaribu kugombea ubunge Kisumu Central kupitia ODM kuelekea uchaguzi wa 2022. Sasa anaandamana na babake kila mahali kama msaidizi wake, hatua inayotafsiriwa kama juhudi ya kuinua wasifu wake na kunufaika na mitandao ya babake.
Kwa Raila Odinga Busia Sankara, mwanasheria kitaaluma, mshikamano wa kifamilia ni jambo la msingi. Akizungumza kwenye mazishi ya shangazi yao Beryl, alisema familia hukutana mara chache sana, hasa wakati wa misiba, na akaomba hilo libadilike.
Hata hivyo, kaka yake mdogo Papa Agolla, ni mwenye msimamo mkali zaidi. Anasisitiza kuwa moto wa kisiasa katika familia utaendelea kuwaka. “Baadhi ya watu wanaweza kuondoka lakini wengine watabaki. Kama mhandisi, ninasema nishati haipotei wala kuumbwa, hubadilika tu. Bado tupo, hatuendi popote,” alisema.
Ndugu mwingine wa Raila, Bw Isaac Omondi Oginga, alisema lengo kuu la kizazi cha sasa cha familia ya Odinga ni umoja. Alisema wanapanga kuwa na mikutano ya mara kwa mara ya kifamilia ili kuendeleza mshikamano ambao marehemu aliwaachia.
Licha ya mikakati ya kufufua nguvu zao, familia ya Odinga bado itakabiliana na migogoro ya ndani na shinikizo kutoka nje yanayolenga kupunguza ushawishi wao wa kisiasa.
Pia yupo dada yao Emily Oginga, Mbunge wa Kuteuliwa katika Bunge la Kaunti ya Kisumu, pamoja na Tabu Osewe, MCA wa North Sakwa Oburu na shemeji wa Dkt Oginga.
Wawili hao ni wapole, lakini wanatarajiwa kuwania nyadhifa kubwa zaidi katika chaguzi zijazo.
Haijabainika iwapo Bi Osewe atatafuta wadhifa wa juu zaidi Kaunti ya Siaya, lakini amewahimiza watoto wa Odinga kuendeleza urithi wa baba yao.
“Tunawapenda sana na tunatarajia kumuona Raila ndani yenu,” alisema Bi Osewe.