Habari

Madaktari wakosoa waliounga ‘miujiza’ ya maombi

Na Elvis Ondieki January 5th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

BARAZA la Madaktari na Wataalamu wa Meno Kenya (KMPDC), ambalo hutoa leseni kwa madaktari, limesuta vikali madaktari waliofika katika mkutano wa injili wa kiongozi wa Kanisa la Repentance and Holiness, Nabii David Owuor, ambapo walithibitisha uponyaji wa wagonjwa mbalimbali kupitia maombi.

Baraza limeahidi kuwa litachukua hatua zinazofaa dhidi ya madaktari hao, ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria.

Kwa washiriki na watazamaji, mkutano huo uliofanyika Desemba 30-31 ulikuwa tukio la kihistoria, kwani watu wenye magonjwa sugu au ulemavu uliokuwa ukiwatatiza walitangazwa kupona.

Hata hivyo, KMPDC imeeleza kuwa kutokuwepo kwa ushahidi wa kisayansi kunasikitisha. Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi na kuthibitishwa na Waziri wa Afya Aden Duale kupitia ukurasa wake katika mtandao wa X, baraza hilo lilikosoa vikali maneno ambayo madaktari walitumia kudai kuwa wagonjwa walipona kupitia maombi.

“Tumepata taarifa za hivi majuzi kwenye vyombo vya habari na mijadala ya umma kuhusu madai ya uponyaji wa imani kwa hali za kiafya, ikiwa ni pamoja na Ukimwi, saratani, upofu, kutatizika kuzungumza na ulemavu wa mwili. Madai haya, yaliyotolewa na baadhi ya wataalamu wa afya wakati wa ibada ya kidini Nakuru, yameibua wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa afya ya umma na maadili ya kitaalamu,” ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa KMPDC, David Kariuki.

“Tunakosoa vikali imani kama hii ya madaktari, inayotokana na madai yasiyothibitishwa,” aliongeza Dkt Kariuki.Baraza lilisema ni muhimu kuzingatia tiba zinazothibitishwa kisayansi.

“Tiba zote lazima ziwe na msingi wa ushahidi wa kisayansi na idhini kutoka mamlaka husika. Madai ya uponyaji wa magonjwa sugu au hatari kama Ukimwi au saratani yanahitaji stakabadhi za kiafya zinazothibitishwa na hayawezi kukubaliwa bila uchunguzi wa madaktari waliohitimu,” iliongeza taarifa hiyo.

“Madai yasiyoweza kuthibitishwa, hasa kutoka kwa wataalamu wa afya, yanaweza kupotosha watu wanyonge na kuwafanya waache kutumia tiba zilizothibitishwa, jambo linaloweza kufanya hali zao kuwa mbaya zaidi, kukataa dawa, au hata kupoteza maisha.”

KMPDC ilionya umma kuwa ingawa imani ina nafasi muhimu katika maisha yao, kutegemea “mbinu za uponyaji zisizothibitishwa” kuna hatari kubwa.

“Tunaonya umma usiache tiba wanazoshauriwa na madaktari kwa zile mbadala zisizothibitishwa, kwani kitendo hicho kinakiuka miongozo ya afya ya umma,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia ilibainisha kuwa uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na mashirika mengine husika.

“Hatua zinazostahili zitachukuliwa dhidi ya yeyote anayehusika ili kulinda afya ya umma, kuheshimu maadili ya tiba na kulinda wananchi dhidi ya taarifa zisizo sahihi,” iliongeza.

KMPDC imesisitiza kuwa mfumo wa afya wa Kenya ni imara, na unahakikisha elimu ya afya ya umma, upatikanaji wa dawa za HIV, huduma za saratani, matibabu ya magonjwa sugu na utafiti wa afya na huduma za kisayansi zinapatikana kwa wote.

Katika mkutano wa injili ulioitwa Menengai 8 Revival Meeting, Nabii Owuor aliwaleta maelfu ya watu Menengai Grounds, wengi wakiwa na ulemavu, wakiomba uponyaji, huku wengine waliokuwa na magonjwa sugu wakihudhuria kwa matumaini ya kupona.