Pombe hatari yahofiwa itawaua vijana milioni moja kabla ya 2030
Na MWANGI MUIRURI
SEKTA haramu ya pombe hatari na ya sumu ikishirikishwa na ufisadi mkuu miongoni mwa baadhi ya maafisa wa usalama ambao baadhi yao wanahusishwa na afisi za hadhi ya juu kabisa, ina uwezo wa kumaliza vijana takriban milioni moja ifikapo mwaka wa 2030, hivyo basi kuhujumu moja kwa moja ajenda kuu za serikali ya Jubilee.
Mauti yakiwa kwa kiwango hicho, itakuwa ni kama haina maana kuwa mbioni kufanikisha ajenda za Rais ambazo ni makao bora, lishe bora, afya bora kwa kila raia, na viwanda kwa kuwa idadi ya walio na nguvu za kushirikishwa kuafikia ajenda hizo kabla ya 2022 ndio wengine walio ndani ya ujana wapate ajira waendelee kujenga Kenya, ndio hao ndani ya vitanda vya mauti.
Ni ulevi ambao tayari Kaunti za Nyandarua, Murang’a na Kiambu zimetaja kuwa janga la Kaunti lakini kwingine serikali kuu na za kaunti hizo zikionekana kutojali, sheria ya kuthibiti hata biashara ya ulevi ikionekana kukiukwa kwa kiwango kikuu.
Kwa mujibu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa mamlaka ya Kupambana dhidi ya Ulevi na Mihadarati (Nacada) John Mututho, pombe hatari inaua vijana 100, 000 kila mwaka, vijana wao hao wakijumlisha utajiri wa Sh15 bilioni kila mwaka kusaka ulevi.
“Hizi ni takwimu ambazo nimeandaa kwa wizara ya masuala ya ndani nikiomba kuwe na mikakati maalum ya kupambana na kero hili. Ni tawimu ambazo tuliandaa kusaidia serikali kupambana na janga hili kati ya 2015 na 2020 lakini hakuna lolote limeonekana kutekelezwa,” akaambia Taifa Leo Dijitali katika mahojiano maalum.
Bw Mututho alisema kuwa uchumi wa taifa kila mwaka hupoteza takriban Sh10 bilioni zaidi katika sekta hii ya pombe za sumu.
“Hizo ni takwimu za kipindi hicho cha hadi 2020 ambapo tulidadisi kuwa uchumi hupoteza Sh5 bilioni kila mwaka kupitia bili za kiafya za waathiriwa wa pombe za sumu huku mauti yakiathiri familia hizo takriban Sh2 bilioni katika kipindi hicho nazo Sh3 bilioni zikipotea kutokana na ukwepaji wa kulipa ushuru kwa serikali kuu,” akasema Bw Mututho.
Bw Mututho aliteta kuwa sekta hii ni vigumu kuithibiti kwa kuwa “imejaa mabwanyenye, maafisa wakuu serikalini na wakora wa kila aina ambao wako na uwezo wa kujikinga dhidi ya mkono wa sheria.”
Alisema kuwa Nacada nayo imetekwa nyara na mitandao ya ufisadi na haina uwezo wowote kwa sasa wa kutekeleza mikakati ya kuokoa taifa dhidi ya ulevi kiholela na unaosihia mauti, akiishutumu kwa kugeuka kuwa fisadi kwa hazina ambazo hupokezwa kupambana na janga hili la ulevi.
“Kwa sasa, wanaoendesha biashara hii ya mauti ni baadhi ya maafisa wa polisi, wengine ndani ya Nacada, walio katika mamlaka ya utoaji leseni katika serikali za Kaunti, baadhi ya wakubwa wa serikali za Kaunti na wafanyabiashara walio na pesa mfukoni kiasi cha kutowajibikia sheria,” akasema.
Bw Mututho alisema kuwa sekta hii ya pombe za sumu huwapa maafisa mafisadi takriban Sh100 milioni kwa siku kupitia hongo.
“Huu ni udadisi ambao ulifanywa na Nacada kwa ushirikiano wa Mpango wa kiusalama wa Nyumba Kumi mwaka wa 2018 ambapo maafisa wa usalama walikuwa wakipokezwa pesa tasilimu na mitandao ya pombe hizo za sumu ili kuilinda dhidi ya mkono wa sheria,” akasema.
Ni ufichuzi ambao aliyekuwa Mkurugenzi wa Nyumba Kumi, Joseph kaguthi anaunga mkono akisema kuwa “kwenye vita dhidi ya pombe za sumu inavunja zaidi ni katika safu ya maafisa wa kiusalama.”
Anasema kuwa “jumbe kutoka mashinani kuhusu urejeo wa pombe za sumu mwaka wote wa 2018 zilionyesha waziwazi kuwa maafisa wa usalama mashinani huzunguka kwa mabaa wakipokezwa hongo ili pombe za sumu ziuzwe bila masharti.”
Anasema kuwa jumbe hizo zilikuwa zikiandamana na hata usajili rasmi wa magari ya polisi ambayo yalikuwa yakinaswa kila jioni yakizunguka mitaani kupokezwa mlungula wa kulinda hata walanguzi wa mihadarati, sio tu washirikishi wa pombe za sumu.
“Hizi ni habari ambazo tulikuwa tunawapasha wakuu wa polisi ili wazishughulikie lakini hakuna la maana lilionekana kutekelezwa na kwa sasa, sekta ya pombe za sumu ni sawa na serikali mashinani,” asema Kaguthi.
Anasema kuwa kwa sasa pesa zile za chini zaidi ambazo afisa aliripotiwa kukabidhiwa ni Sh200 ili alinde biashara hiyo ya pombe za sumu huku kukiwa na hongo ya Sh250, 000 ambayo ilidaiwa katika Mji wa Subukia mwaka wa 2016 ili baa ya kuuza chang’aa ipewe leseni ya kuhudumu hadharani, na ambapo ilipewa.
Aidha, Bw Kaguthi anasema kuwa kwa sasa kuna madiwani, maafisa wa polisi na hata wandani wa wanasiasa ambao wamefungua biashara haramu za kupika pombe bila kufuata utaratibu wa sheria za nchi hasa kuhusu afya kwa binadamu, na hakuna vile kunaweza tekelezwa sheria ya kuwaandama.
“Serikali itaiandama serikali kwa njia gani? Si Rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2015 alizindua vita dhidi ya pombe hizo za sumu lakini hata kabla ya mwaka kuisha, pombe hizo zikawa zimerejea sokoni? Hii ni serikali kusema imezima biashara hiyo katika soko la Kusini lakini kule Kaskazini, inafungua biashara iyo hiyo,” akasema.
Kwa mujibu wa gavana wa Nyandarua, Francis Kimemia, “kati ya mwaka wa 2004 na 2016 nilikuwa ndani ya wizara ya usalama wa ndani na ninaweza nikakwambia kwa uhakika kuwa sekta ya pombe haramu huwa ni mtandao sawa na mafia katika mataifa ya ng’ambo kama Colombia na Italia.”
Anasema kuwa serikali hadi sasa imeorodhesha sekta hiyo ya pombe za sumu kama janga la kitaifa, akisema kuwa “ni sekta ambayo inafaa kuwekewa mikakati mfululizo ya kuwaandama wote walio ndani ya biashara hiyo.”
Anasema kuwa serikali iko na sera maalum ambayo inataja pombe za sumu kuwa “sekta ya mauti nchini Kenya” na ambapo kila Kamishna wa Kaunti anaelewa kuwa jukumu lake la kwanza ni kupambana na pombe zote aina ya takataka.
“Lakini nasikitika kwa kuwa sasa niko katika siasa na ninashuhudia moja kwa moja jinsi sera hiyo ya serikali huhujumiwa kimakusudi. Kuna maafisa nyanjani ambao haja yao ni kupokezwa pesa kidogo na wanaachilia pombe za kila aina kuuziwa wateja. Matokeo ni kuwa vijana wengi wanaaga dunia mapema chini ya athari za pombe hizi,” asema.
Nguvu
Mwenzake wa Kiambu, Ferdinand Waititu anasema kuwa ana ufahamu wa jinsi mtandao huo wa pombe za sumu huwa na nguvu kama ya kiserikali.
“Ni sekta ambayo gharama zake za uzalishaji ni Sh20 kwa kila Sh100 ambazo wanapata. Faida ni Sh80 katika mauzo ya Sh100. Hiyo ni faida ya juu hata kuliko hata kampuni tajika za kibiashara hapa nchini. Utajiri huo hugawanwa katika mtandao huo wa kibiashara na maafisa wa kiusalama pamoja na baadhi ya walio ndani ya kuunda sera,” asema Waititu.
Anasema kuwa mtandao huo wa ufisadi ndani ya pombe za sumu hufadhili kwa mamilioni ya pesa karamu za kufunga mwaka katika vituo vingi vya polisi hapa nchini ambapo hata mifugo huchinjwa, wali na chapati kuzidi maafisa na pombe kuwalemea maafisa hao uskiu mzima wa raha hiyo.
Anaonya kuwa ni mtandao ambao huwa tayari kujiingiza hata katika ushindani wa kisiasa kwa kuwa “uko na pesa na pia ufuasi ndani ya walevi ambao wamatekwa nyara katika kashfa hiyo ya mauti, pamoja na wale ambao wamefungua mabaa wakigeuka pia kuwa wafuasi wa mtandao huo.
“Ndiyo sababu mtandao huo ukianza kukulenga kukuangamiza kisiasa, usiku mmoja tu unatosha habari zako mbaya ziwe zimesambaa kote nchini. Wafanyabiashara hao watatumia mtandao wao wa uteja na ulinzi ndani ya serikali kusambaza jumbe hizo kwa kasi mashinani,” asema.
Mututho anasema kuwa hivyo ndivyo alianguka kura ya ubunge Naivasha mwaka wa 2013 na kisha akaanguka ya Ugavana mwaka wa 2017 katika Kaunti ya Nakuru kwa kuhusishwa na Sheria ya kuthibiti biashara ya pombe ya 2007 maarufu kama ‘Sheria ya Mututho.’