Habari za Kitaifa

Mwalimu aliyefutwa kazi kwa kuhepa hatari Mandera ashinda kesi

Na WINNIE ATIENO January 9th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

KWA takribani miaka mitatu, mwalimu Geoffrey Lelon alikuwa akipambana katika mahakama baada ya kusimamishwa kazi.

Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) ilichukua hatua hiyo ikimlaumu mwalimu huyo wa Jiografia na Historia kwa kuhepa kazi alipotoroka eneo la Kaskazini Mashariki lililojaa vitisho ili kuokoa maisha yake.

Hata hivyo, mnamo Desemba 4, 2025, kile Lelon alichotaja kama “kifungo” hatimaye kilifunguliwa. Katika uamuzi wa kihistoria uliotolewa na Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya Milimani, Jaji Byram Ongaya aliamuru Lelon atumwe mara moja kituo salama cha kazi.

Tangu 2023, mwalimu huyo alikuwa akiomba kuhamishiwa kituo salama baada ya kutoroka Kaskazini Mashariki.

Uamuzi wa Jaji Ongaya ulikuwa wazi. Mahakama ilizingatia historia ya kesi na hatari zilizomkabili na kuagiza TSC kuondoa hatua ya kumsimamisha kazi Lelon na kumhamisha kutoka Kaskazini Mashariki anakokabiliwa na hatari kwa maisha yake.

“Mahakama imezingatia historia ya kesi na ushahidi uliopo na kuagiza TSC kumhamisha mwalimu Geoffrey Lelon kutoka Kaskazini Mashariki hadi shule nyingine yoyote mara moja ili aanze kazi muhula ujao,” ulisema uamuzi wa Mahakama, huku Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC akiagizwa kuutekeleza.

Mahakama pia ilionya kuwa kutakuwa na adhabu endapo agizo hilo halitatekelezwa.

Kwa Lelon, uamuzi huo unamaanisha kuwa anapoanza muhula wa 2026, ataacha nyuma hofu ya vilipuzi na kurejea darasani katika mazingira salama.

Safari yake kuelekea ushindi huo imejaa maumivu. Awali, alifurahia kupelekwa Shule ya Sekondari ya Duse Boys, Mandera Mashariki, lakini aligundua haraka kuwa kufundisha Kaskazini Mashariki kulihitaji zaidi ya taaluma—kulihitaji mbinu za kuishi.

Walimu walilazimika kulala katika vituo vya polisi wakihofia mashambulizi ya Al-Shabaab, huku Lelon akishuhudia magari yaliyoharibiwa na vilipuzi na kuuawa kwa mwenzake Philemon Ngeno mnamo 2023.

Baada ya walimu zaidi ya 100 kutoroka eneo hilo 2023, TSC ilikataa kuwahamisha na kuwasimamisha kazi walimu 60.