Kinaya mahakama sasa ikiomba NG-CDF pesa za kujenga korti
BAADA ya kutangaza Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) kuwa kinyume cha katiba na kutoa agizo kwamba ifungwe kufikia Juni 30, 2026, sasa Mahakama inaomba Bunge kuhakikisha sehemu ya pesa za hazina hiyo zinatumika kusaidia ujenzi wa mahakama kote nchini.
Ombi hilo limewasilishwa kwa wabunge kwa sababu ya “ukosefu wa ufadhili wa kutosha” kwa mahakama, ambapo bajeti iliyotengwa ni chini ya asilimia moja ya bajeti ya taifa licha ya kukabiliana na mzigo mkubwa wa kesi 257,000.”
Stakabadhi zilizopatikana na Taifa Leo zinaonyesha Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), Isaac Ruto, aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Bomet, alitoa ombi hilo kwa Kamati ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Katiba (CIOC) ya Bunge la Kitaifa.
“JSC ilitoa pendekezo kwa bunge kuzingatia kutenga sehemu ya NG-CDF kusaidia ujenzi wa mahakama kote nchini,” Bw Ruto alisema katika stakabadhi ya JSC iliyotolewa kwa CIOC, inayosimamiwa na Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi.