Habari

Jaji Njoki Ndung’u achaguliwa kuwasilisha mahakama ya juu ya JSC

January 10th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

JAJI Njoki Ndung’u amechaguliwa kuwa mwakilishi wa Mahakama ya Juu katika tume ya kuajiri watumishi katika idara ya mahakama (JSC).

Jaji Ndung’u alichaguliwa bila kupingwa mnamo Januari 9,2026 kutwaa mahala pa marehemu Jaji Mohammed Ibrahim aliyeaga Desemba 17,2025 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Jaji Ibrahim alihudumu kama mwanachama wa JSC tangu alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu 2011.

Hadi kifo chake Jaji Ibrahim alikuwa Jaji wa Mahakama ya Juu na wakati huo huo mwakilishi wa korti hii ya upeo katika JSC.

Majukumu hayo mawili yalimwezesha Jaji Ibrahim kuhakikisha ubora wa utekelezaji wa Katiba sawia na unyoofu wa utenda kazi katika idara ya mahakama kupitia JSC.

Jaji Ndung’u alichaguliwa katika hafla iliyowajumuisha Jaji Mkuu (CJ) Martha Koome , Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu ,Jaji Smokin Wanjala Jaji Isack Lenaola na Jaji William Ouko.

Zoezi hilo liliongozwa na Afisa wa Kusimamia Uchaguzi kutoka tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Dkt Swallah Yusuf.

Jaji Ndung’u alichaguliwa kwa mujibu wa mwongozo na Sheria za JSC za 2011 zinazoitaka Idara ya Mahakama ya Juu kuwasilisha mwakilishi wake katika muda wa siku 21 baada ya mwanya kuimbuka.

Jaji Ndung’u anayetwaa nafasi ya mwendazake Jaji Ibrahim ametambulika katika mchango wake wa kutetea haki za binadamu na masuala ya jinsia nchini.

Mbali na wadhifa huo mpya , Jaji Ndung’u pia ndiye mwenyekiti wa kamati ya idara ya mahakama kuhusu uchaguzi na uteteaji wa haki za wafanyakazi katika idara ya mahakama.

Katika hotuba yake baada ya kuchaguliwa Jaji Ndung’u aliahidi kutekeleza majukumu yake bila woga, upendeleo na kuhakikisha haki imetendeka.

“Nitatekeleza majukumu yangu kwa uwazi, kuhakikisha haki imetendeka na kushinikiza uhuru wa idara ya mahakama katika utekelezaji wa kazi zake,” Jaji Ndung’u alisema.

Akimpongeza Jaji Ndung’u kwa uteuzi wake Jaji Koome, aliyepia mwenyekiti wa JSC, alisema yuko na imani naye na kuongeza ,”mchango wako kutetea haki za jinsia na utekelezaji wa katiba umetambulikana kote.”

Jaji Koome aliwataka wakenya wajitokeze kutetea haki zao na za wengine bila woga.

Baada ya kifo cha Jaji Ibrahim, mahakama hii ya upeo imesalia na majaji sita ambao ni Jaji Koome, Jaji Mwilu, Jaji Wanjala, Jaji Ndung’u, Jaji Lenaola na Jaji Ouko.

Zoezi la kuteuliwa kwa Jaji mwingine kutwaa wadhifa wa Jaji Ibrahim bado kutangazwa na JSC.

Atakayeteuliwa sharti awe amehudumu kama Jaji wa Mahakama kuu , Mahakama ya Rufaa ama ametekeleza majukumu ya wakili kwa zaidi ya miaka 10 tangu ahitimu chuo kikuu kwa shahada ya digirii masuala ya sheria.