Gachagua adai maisha yake yamo hatarini baada ya kushambuliwa
ALIYEKUWA Naibu Rais, Rigathi Gachagua Ijumaa, Januari 9, 2026, alidai kuwa maisha yake yako hatarini baada ya polisi kujaribu kumzuia kuingia Kaunti ya Kirinyaga.
Katika eneo la Sagana, maafisa wa polisi waliokuwa na silaha walizuia msafara wa Bw Gachagua alipokuwa akielekea Kagio kuhutubia mkutano wa kisiasa wa chama cha DCP kando ya barabara.
Kulizuka taharuki huku Bw Gachagua na wandani wake wakikimbilia usalama wao. Wakati wa mkanganyiko huo, baadhi ya magari yaliyokuwa katika msafara wake yaliharibiwa.
Kiongozi huyo wa DCP na wafuasi wake walilazimika kutumia njia ndefu kupitia Kandongu hadi mji wa Kagio, ambako walipokelewa na maelfu ya wafuasi.
Hali ya wasiwasi ilitanda Kagio huku polisi waliokuwa na silaha nzito wakipiga doria mjini humo, hata hivyo Bw Gachagua aliendelea na mkutano wake bila woga.
“Walitupiga kwa vitoa machozi na wakatufyatulia risasi,” aliwaambia wafuasi wake katika mji wa Kagio, eneo la Ndia, akidai maisha yake yako hatarini.
Aliapa kuwa hakuna vitisho vitakavyomzuia kuzuru kila pembe ya kaunti hiyo au kubadili mwelekeo wa kisiasa wa wakazi wa Kirinyaga.
“Serikali ya Kenya Kwanza ina wasiwasi kwa sababu ninasema ukweli kwa Wakenya, ndiyo maana polisi wanatumwa kunishambulia mimi na wafuasi wangu,” alisema Bw Gachagua.
Bw Gachagua alisema juhudi zake za kumng’oa Rais William Ruto kidemokrasia katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 haziwezi kuzuiwa.
“Nitahakikisha Ruto anakuwa rais wa muhula mmoja,” alisema.
Aliendelea kumshutumu Rais Ruto kwa kuharibu uchumi wa nchi kwa gharama ya wananchi.
“Rais Ruto ameharibu uchumi na kwa kushirikiana na wenzangu wa upinzani tutampeleka nyumbani,” alisema.
Alimlaumu Rais kwa kudai kuwa ana uwezo wa kuigeuza Kenya kuwa Singapore.
“Kile Ruto ametuambia ni cha kuchekesha, tunapaswa kumcheka,” alisema.
Bw Gachagua aliandamana na Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala, Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango, Seneta wa Nyandarua John Methu pamoja na viongozi wengine.
Awali, akiwa mjini Nyeri alipokuwa akizungumza na wanahabari, Bw Gachagua alitoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa kuhusu zoezi tata la uteuzi wa wanafunzi wa Gredi ya 10, akisisitiza kuwa zoezi hilo limeegemea baadhi ya maeneo.
Alitetea kauli zake za awali kuhusu wanafunzi “kutoka nje” kupelekwa katika shule za Mlima Kenya, akisema wanafunzi wa eneo la Kati pia wana haki ya kusoma katika shule bora.
Alihoji kuwa baadhi ya maeneo yamepokea mabilioni ya fedha kupitia hazina ya usawazishaji tangu ugatuzi uanze lakini hayajajenga shule bora, ilhali viongozi wake wanamshambulia anapodai haki katika fursa za elimu.
Alisisitiza kuwa wanafunzi wa Gredi 10 kutoka baadhi ya maeneo wanapaswa kupewa kipaumbele katika uteuzi.
“Watoto wote nchini ni sawa, lakini watoto wa eneo hili wanapaswa kupewa kipaumbele bila kuwabagua wale wa maeneo mengine,” alisema.
Alikanusha madai kuwa kauli zake ni za kikabila, akisisitiza kuwa uteuzi wa wanafunzi katika shule za kitaifa unapaswa kufanywa kwa uwazi na haki.
Bw Gachagua aliwaambia wanaomkosoa kwa kuwa “mkali” kuhusu masuala ya Mlima Kenya kwamba hatanyamaza huku Rais Ruto akidaiwa kusababisha mkanganyiko katika sekta ya elimu.
Alitaja Kaskazini mwa Kenya kama eneo lililopokea mabilioni ya fedha lakini viongozi wake wameshindwa kuendeleza shule bora za kitaifa.
“Tunahitaji mazungumzo ya kitaifa kuhusu suala hili la uteuzi. Watu wa Kaskazini Mashariki ndio hunishutumu kwa ukabila ilhali wana fedha lakini hawajajenga shule bora kwa watu wao,” alisema.
Alhamisi, Rais Ruto alimshutumu Gachagua kwa kueneza siasa za chuki na ukabila kuhusu mfumo wa elimu.
“Sasa wameenda hadi shuleni kugawanya watoto wetu. Mmefikia kiwango gani cha kukata tamaa? Waacheni watoto wetu wasome. Watoto hao ni Wakenya bila kujali jamii wanayotoka,” alisema Rais.
Viongozi kadhaa wanaoegemea UDA wamejitokeza kutetea uteuzi wa wanafunzi.