Jamvi La Siasa

KINAYA: Wasanii wa Tanzania watakula jeuri yao baada ya kuunga CCM

January 11th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HIVI ajali ya barabarani ikatokea saa hii ikimhusisha ng’ombe na binadamu, utampa yupi pole na kumtakia afueni ya haraka?

Bila shaka pole na sala zote ni kwa binadamu. Ng’ombe tunamgeuza nyama mara moja kwa kuwa kupona kwake hakuna manufaa mengi kwetu.

Hata hivyo, mara nyingine mambo hayaendi yanavyotarajiwa. Hivi majuzi nchini Tanzania, ajali ambapo msanii kwa jina Shilole amemgonga ng’ombe kwa gari lake.

Badala ya watu kumpa pole msanii wao, wengi walikimbia kwenye mitandao ya kijamii kumtolea pole ng’ombe huyo wasiyemjua, wakamtakia nafuu ya haraka.

Shilole naye? Potelea mbali! Akutane na ya kumkuta eti, tena pole zake apewe na Chama (tawala) Cha Mapinduzi (CCM)!

Hivi utakuwa umewafanyia watu kitu gani ndio wamliwaze ng’ombe kukuzidi? Kwani hawapendi nyama ya ng’ombe ilhali wewe binadamu ukifa hawatakula?

Thamani ya uhai wa binadamu imeenda wapi? Labda binadamu mwenyewe ajithamini kwanza.

Watanzania wamechoshwa na kuchushwa na wasanii wao ambao wanaiunga mkono serikali dhalimu ya CCM ambayo iliwaua maelfu ya watu walioandamana kupinga ukandamizaji na uchafuzi wa uchaguzi mwishoni mwa mwaka jana.

Wasanii hao, ambao wametajirika haraka kwa kushabikiwa na wananchi wa kawaida, walichemsha pakubwa walipopuuza dhuluma na mateso waliyofanyiwa raia na kufungamana na kachinja Suluhu Hassan.

Baadhi yao, kama Diamond Platinumz niliyemshabikia si haba, walijitokeza na kulaani maandamano, hata wakawadharau waandamanaji kwa kuwaita wazembe wasiotaka kufanya kazi.

Sasa kinawaramba kweli kwa sababu hakuna anayetaka miziki yao hiyo, mashabiki wameacha kuwafuata mtandaoni, hakuna anayetaka shoo zao, nasi huku nje tunatazama sinema yenyewe kwa tabasamu ya mwaka na mafunda makubwa ya vinywaji tuvipendavyo.

Serikali yao inawaambia mashabiki watofautishe kazi na siasa na kazi, eti muziki ni kazi kama nyingineyo ambayo kwayo msanii anatia tonge kinywani, lakini Watanzania wameshupaa!

Hakuna msanii anayeweza kuandaa shoo yoyote hata kwenye baa ya kijijini kwao kwa kuwa walikataa kutumia akili na kuonyesha huruma ilipohitajika zaidi.

Hata mashabiki Wakenya wamewakataa. Juzi nimeona waliozoea kupitia mpakani Lungalunga na kuingia Kenya, hasa pwani, na kutumbuiza huko wakiambiwa wathubutu kufanya hivyo ili wajue kilichomtoa kanga manyoya!

Wanasiasa wa pwani ya Kenya waliozoea kujizolea umaarufu kwa kuwaleta wasanii wa Tanzania nchini wametishiwa kutiwa adabu.

Sijui kwa mijeledi, mawe, kutemewa mate, kumwagiliwa maji ya chumvi au kunyimwa kura, lakini wametishiwa.

Binafsi, tangu zamani shabiki mkuu wa wasanii wa Tanzania, nimefuta nyimbo zao na kuacha kuwafuata mtandaoni kwa kuwa sijakolewa na uzuzu kiasi cha kuwa na ubia na watu wanaotumia ubongo kukinga shingo na jua.

Kama tusemavyo Kenya, wasanii wa Tanzania watakula ujeuri wao kwa sababu wamevimba vichwa hivi kwamba hawawezi kufanya kitu rahisi kama kuomba msamaha. Kiburi kina gharama kumbe?

-Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika ([email protected])