Dimba

AFCON2025: Morocco na Senegal teketeke nusu fainali

Na MASHIRIKA January 11th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA wa Morocco, Walid Regragui, alikana vikali madai kwamba refa aliwasaidia katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Cameroon kwenye robo-fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) 2025 mnamo Ijumaa usiku.

Kwenye mechi nyingine Senegal walishinda Mali 1-0 kufuzu nusu-fainali.

Mali walicheza kipindi cha pili watu 10 uwanjani baada ya Yves Bissouma kuonyesha kadi ya pili ya manjano na hivyo ikawa nyekundu dakika ya 45+3.

Kocha wa Morocco, Regragui, alisema Atlas Lions walishinda mchuano huo kutokana na juhudi na mchezo mzuri wala si kutokana na kusaidiwa na refa.

“Tulistahili kupata ushindi. Ukitaka kumuua mbwa wako bila sababu, huwa unasema kwamba ana kichaa,” akasema Regragui.

Mchezaji huyo wa zamani wa Morocco alisema wanasoka wake walipata ushindi huo kwa haki na kupambana uwanjani, akikanusha kuwa kulikuwa na mkono wa refa.

“Hakuna bao ambalo Cameroon walifunga na refa akakataa. Watu wanataka kusawiri mchezo huo kana kwamba tulisaidiwa na refa ilhali sisi hushinda mechi zetu uwanjani,” akaongeza huku akionekana kuchemka sana.

Baada ya kuipiga Cameroon 2-0 wenyeji hao wa AFCON con sasa watacheza na mshindi kati ya Nigeria na Algeria ambayo ilikuwa isakatwe Jumamosi jioni.

Kwenye mtanange huo mabao ya Morocco yalifungwa na Brahim Diaz na Ismael Saibari.

Diaz, 26 ambaye anasakatia Real Madrid, sasa amefunga mabao matano katika Afcon ya mwaka huu.

Senegal nao walihitaji bao la kipindi cha kwanza cha Ilman Ndiaye kushinda Mali kwenye Debi ya Afrika Magharibi.

Eagles walipata pigo dakika ya tatu muda wa ziada kipindi cha kwanza baada ya Yves Bissouma kupewa kadi nyekundu.

Sadio Mané, Pathé Ciss na Lamine Camara walikosa nafasi kadhaa za kufunga mabao ambazo zingesaidia Senegal kupata ushindi mkubwa katika mechi hiyo.

Senegal walikuwa wanasubiri kufahamu mpinzani wao katika pambano la robo fainali ambalo lilikutanisha mabingwa watetezi Cote d’Ivoire na Misri baadaye jana usiku.

Kocha wa Senegal Pape Thiaw alisema kuwa alitarajia wangefunga mabao mengi dhidi ya Mali.

“Haikuwa mechi rahisi kwa sababu tulicheza dhidi ya Mali ambayo ina timu nzuri na ilibuni nafasi kadhaa za kufunga hata kama walikuwa wachezaji 10,” akasema Thiaw.

“Nilitarajia tungemakinika zaidi mbeleni mwa lango na tufunge mabao mengi. Hata hivyo, nimefurahi tumefuzu nusu fainali kwa sababu macho yetu yapo katika kutwaa kombe hili,” akaongeza.