Lugha, Fasihi na Elimu

ELIMU MSINGI: Rotich, mwalimu mwenye siri kubwa ya ufanisi

Na RICHARD MAOSI January 12th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MWALIMU aliye na wito wa kufundisha na mapenzi ya dhati kwa taaluma yake ana jukumu zito la kuchochea wanafunzi wake kupiga hatua kubwa katika safari ya elimu inayohitaji subira, kujinyima kwingi na moyo wa kujitolea.

Zaidi ya kufahamu wanafunzi wake kwa majina, mwalimu bora pia sharti awe na bidii na msukumo wa kutaka kujifunza mambo mapya.

Awe mwepesi wa kuchangamkia masuala yanayofungamana na mtaala na asome kutoka kwa vyanzo mbalimbali ili awe chemchemi ya maarifa kwa wanafunzi wanaomtegemea darasani.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Darius Kibet Rotich ambaye kwa sasa ni mwalimu katika Shule ya Upili ya Lelwak Boys iliyoko Kapsabet, Kaunti ya Nandi.

Kwa mtazamo wake, mwalimu bora lazima ajitahidi kuhudhuria vipindi vyote vya somo lake, awe mnyumbufu katika maandalizi ya vipindi hivyo na mbunifu katika uwasilishaji wa anachokifundisha.

“Atoe mazoezi ya kutosha kwa wanafunzi, arejeshe masahihisho ya kazi zao mapema na awape matokeo ya mitihani kwa wakati unaofaa. Anastahili pia kutumia nyenzo mbalimbali za ufundishaji ambazo zitateka saikolojia ya wanafunzi wake haraka, kuwaamshia ari ya kuthamini masomo na kukuza vipaji vyao katika ngazi na viwango tofauti,” anasema.

Darius alilelewa katika eneo la Koilot, Nandi Mashariki. Ndiye wa tano kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bi Salina Cheruto na mwalimu mstaafu Bw Samuel Rotich.

Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi ya Kipkoror, Nandi (2006-2011) kabla ya kupitia katika Shule ya Msingi ya Kibabet, Nandi (2012-2013) kisha Shule ya Upili ya Baringo iliyoko Ravine (2014-2017). Ana shahada ya ualimu (Kiswahili/Dini) kutoka Chuo Kikuu cha Moi (2018-2023).

Ingawa matamanio yake kuanzia utotoni yalikuwa kujitosa katika ulingo wa utabibu, alihiari mwishowe kusomea ualimu baada ya kuchochewa na baba mzazi pamoja na Bw Robert Kimatep ambaye alimfundisha Kiswahili katika shule ya sekondari.

Kati ya waliokuwa wakimpigia mhuri wa kuwa daktari hapo awali ni Bi Leah Serem ambaye alimpokeza malezi bora zaidi ya kiakademia katika Shule ya Msingi ya Kipkoror.

“Walimu wangu walikuwa walezi wema wa vipaji vya wanafunzi na washauri wa kutegemewa hata katika masuala yasiyohusiana moja kwa moja na masomo. Walijali maslahi ya wanagenzi wao na wakawa mstari wa mbele kutambua matatizo yao, kuelewa kiwango cha mahitaji ya kila mmoja wao na kusuluhisha changamoto zao ipasavyo,” anaeleza.

Kabla ya kuhitimu chuoni, Bw Darius alishiriki mafunzo ya nyanjani mnamo 2022 katika Shule ya Upili ya Saroiyot iliyoko viungani mwa jiji la Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Aliajiriwa baadaye katika shule hiyo kwa muda mfupi mnamo 2023 kabla ya kupata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Upili ya Alungo iliyoko Seme, Kaunti ya Kisumu (2023-2024).

Alitua Lelwak Boys mnamo Mei 2025 na akaaminiwa kuwa kocha msaidizi wa mchezo wa unyoya (badminton).

Bw Darius anahimiza walimu kutolinganisha mishahara yao na kazi kubwa muhimu wanazozifanya.

Wito wake kwa wote wanaoingia uongozini ni kuwa na utu, wawajibikaji na watekelezaji wa majukumu yao kwa kujituma bila kushurutishwa na yeyote.