Joho na Achani watofautiana kuhusu madini ya Mrima Hills
MVUTANO umeibuka kati ya viongozi wa Kaunti ya Kwale na Serikali ya Kitaifa kuhusu mipango ya kuanzisha shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la Mrima Hills.
Viongozi wa kaunti hiyo wakiongozwa na Gavana Fatuma Achani, pamoja na wakazi na mashirika ya jamii, wametaka kuhusishwa kikamilifu katika mchakato mzima.
Hali ya wasiwasi imetokana na namna Serikali ya Kitaifa ilivyoshindwa kuwasilisha mabilioni ya pesa yaliyopatikana kutokana na shughuli za kampuni ya Base Titanium kwa kaunti na jamii zilizopakana nayo, pamoja na hofu ya jamii kuhamishwa.
Base Titanium ilisimamisha shughuli zake mwaka wa 2024 baada ya kumaliza kuchimba madini yaliyolengwa katika eneo hilo.
Katika kikao cha mashauriano kilichoandaliwa na Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Hassan Joho, wiki iliyopita, viongozi hao walisema hawatakubali kudanganywa.
Viongozi walisema shughuli za uchimbaji madini zinaweza kuathiri maisha ya wananchi na maeneo ya kitamaduni yanayozunguka Mrima Hills.
Naibu Gavana wa Kaunti ya Kwale, Bw Josphat Chirema, aliondoka katika kikao hicho cha Ijumaa kilichoandaliwa Matuga akiwa pamoja na viongozi wengine wa eneo hilo.
Walilalamika kuwa Serikali ya Kitaifa inawalazimisha wakazi kuunga mkono mradi huo bila uwazi.
“Hatuwezi kukaa katika kikao ambacho viongozi wanatishwa na kunyimwa fursa ya kuwasilisha hoja za wananchi wanaowawakilisha. Mchakato huu una dosari na unadharau uongozi wa Kaunti ya Kwale,” alisema Bw Chirema.
Jumamosi, Gavana wa Kaunti ya Kwale, Bi Fatuma Achani, aliandaa kikao tofauti pamoja na wakazi na viongozi kuhusu suala hilo hilo.
Bi Achani alisisitiza kuwa, hakuna uchimbaji wa madini utakaofanyika hadi mashauriano ya kina na wadau wote yatakapokamilika.
“Ninawaomba wakazi wabaki watulivu kwa sababu kwa sasa hakuna mipango ya kuendelea na uchimbaji wa madini hadi Serikali ya Kitaifa itakapoafikia makubaliano na jamii za eneo hili,” alisema.
“Ninawaomba viongozi wote, iwe ni wa serikali au wazee wa Kaya, kutofanya mikutano yoyote kinyume na matakwa ya wakazi wa Mrima. Dzombo ni makazi ya watu wengi,” aliongeza gavana huyo.
Bw Joho hapo awali alikuwa amelaumu uenezaji wa taarifa potovu uliosababisha upinzani dhidi ya mradi wa madini.
Kwa mujibu wa waziri huyo, mipango ya uchimbaji madini Mrima Hills ilikuwa bado katika hatua za awali, lakini umma ulikuwa umefanywa kuamini kuwa mradi huo ulikuwa tayari umeafikia hatua zinazohitaji kuwahamisha wakazi na kuwalipa fidia.
“Kuna uvumi mwingi unaosambaa kuhusu mradi huu. Bado hatujatambua hata kampuni itakayofanya utafiti wa awali ili kubaini kiwango halisi cha madini, ukubwa wa mradi na taarifa nyingine muhimu zitakazotoa mwelekeo wa hatua zinazofuata,” alisema.
Bw Joho aliongeza kuwa, taarifa potovu zilizoongeza hofu miongoni mwa wakazi ndizo zilimlazimu kuitisha kikao hicho ili kusikiliza moja kwa moja sauti za wananchi, ambao waliibua masuala kuhusu fidia, ulinzi wa mazingira na namna faida za uchimbaji madini zitakavyogawanywa.
Waziri alisema serikali haitaruhusu njia za mkato katika miradi ya uchimbaji madini, akisisitiza kuwa sheria lazima ifuatwe na jamii zilindwe dhidi ya madhara.
Mrima Hills ni mojawapo ya maeneo duniani yanayojulikana kuwa na madini adimu, ikiwemo niobium.
Eneo hilo limevutia mataifa mbalimbali ya kigeni kwa miongo kadhaa, yakiwemo Japan, China na Marekani.
Mnamo Aprili mwaka jana, muungano wa makampuni mawili yaliyosajiliwa katika Soko la Hisa la Australia, RareX na Iluka Resources, uliwasilisha maombi kwa Shirika la Kitaifa la Madini la Kenya kuomba haki za utafiti wa madini katika Mrima Hill, Kaunti ya Kwale.
Mwaka 2012, kampuni ya Cortec Mining Kenya Ltd ilifanya Tathmini ya Athari za Mazingira na kuwasilisha ripoti kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya uchimbaji wa niobiamu na madini adimu katika Mrima Hill, lakini ripoti hiyo ilikataliwa.
Kampuni hiyo ilikadiria kuna madini ya thamani ya Sh12.9 trilioni.
Mahitaji ya kimataifa ya niobium, inayotumika kuimarisha chuma, yanaongezeka kwa kasi ulimwenguni.