Mume anaficha simu yake kama bangi hata saa za kulala anaiweka chini ya godoro!
Mume wangu analala na simu chini ya mto. Hata bafuni anaingia nayo. Nikimuuliza ananiambia nina wivu. Nifanyeje?
Simu ikiwa muhimu kuliko mke, hapo kuna jambo. Usianze upelelezi ila kaa naye chini muzungumze wazi. Kama hana cha kuficha, hatakataa mazungumzo.
Lakini kumbuka: heshima huanza kwa mawasiliano, sio kuchungulia WhatsApp ya mwenzako.
Rafiki yangu ameolewa ila ana dume la pembeni, nitoboe siri au nifyate domo?
Niko na rafiki yangu wa dhati ambaye ameolewa, lakini pia ako na mpenzi mwingine wa pembeni. Amekuwa katika ndoa na huyo mumewe sasa ni zaidi ya miaka 5. Je, nimweleze mume wake kuhusu siri hiyo au nifyate mdomo.
Kabla ya kuchukua hatua yoyote ile inayoweza kuwakosanisha, zungumza na rafiki yako kwa upole na umshauri. Kumshtaki kwa mume wake moja kwa moja kunaweza kukuingiza kwenye mgogoro.
Nilikuwa changaduo hapo zamani na sasa nimepata mwanamume ninayependa
Vipi Shangazi. Hapo nyuma nilikuwa kahaba lakini sasa nimebadilika. Kwa sasa kuna mwanaume ninayempenda sana na sijui ikiwa ni busara kumjulisha maisha yangu ya kitambo.
Kila mtu ana historia, lakini sio kila historia inahitaji kutangazwa hadharani. Ikiwa maisha yako ya sasa ni mapya na umebadilika kweli, basi tafakari kwa makini kabla ya kufichua.
Mweleze tu ikiwa uaminifu wako kwake uko hatarini au unahisi anaweza jifunza kutoka kwako. La sivyo, endelea kuishi maisha ya sasa kwa heshima, uaminifu na toba ya kweli.
Kuna mtindo chwara naona kwa mpenzi wangu, huwa anapotea mwisho wa mwezi
Shangazi, kila mwezi baada ya kupata mshahara mpenzi wangu huwa amejaa pesa. Lakini huwa anapotea kama mtandao wa simu kule ushago. Hurejea tu baada ya hela kumuishia. Huu ni upendo?
Huo si upendo. Jiulize iwapo anakupenda au anapenda mshahara wake? Mapenzi ya kweli sio ya ‘Mteja hapatikani…’ wakati ana hela.