Polisi waliompiga risasi na kuua kijana Gen Z mtaani Mukuru kusota rumande
MAAFISA wawili wa polisi waliompiga risasi na kumuua mwanaume wa miaka 20 katika eneo la Mukuru kwa Njenga wameagizwa wakae rumande wa siku 14 kuhojiwa kubaini sababu ya kutekeleza uhalifu huo.
Sajini Godwin Mjomba na Konstebo Patrick Mutunga Titus waliamriwa wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Capital Hill hadi Januari 26, 2026.
Akiamuru wawili hao watupwe rumande, hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Carolyne Nyaguthii Mugo, alisema mauaji ya Shukri Adan Ibrahim Issaka mnamo Januari 11, 2026 yalikera umma na kusababisha maandamano na uharibifu wa mali.
Hakimu alikubaliana na mamlaka huru ya polisi IPOA kwamba sharti uchunguzi wa kina ufanywe kubaini sababu ya Shukri kuuawa kinyama.
Naibu Mkurugenzi wa Masuala ya Uchunguzi IPOA Abdirahaman Jibril alimweleza hakimu kwamba kulikuwa na njama za kuficha mauaji hayo ya Shukri na maafisa wa polisi kutoka kituo cha Villa kilichoko eneo la Mukuru kwa Njenga eneo la Embakasi kaunti ya Nairobi.
Shukri aliuliwa katika eneo la MCC mwendo wa saa 12 na dakika 10 asubuhi.
Kabla ya kuuawa Shukri, mahakama ilielezwa alikuwa ameandamana na Wycliffe Nyakwama na Festus Mutinda.
Watatu hao walikuwa wanaipeleka gari namba ya usajili KDN 266B muundo wa Toyota Fielder kwa Bw Joho katika mtaa wa Imara Daima.
Wakiwa njiani mahakama iliambiwa gari hilo liligongana na gari la abiria-Matatu ndipo vurumai na mtafaruku vikazuka.
Mahakama ilielezwa ni wakati huo maafisa hao polisi walifika na kuwaamuru Shukri, Nyakwama na Mutinda walale chini.
“Shukri alipigwa risasi ya kichwa na kufa papo hapo,” Jibril alieleza mahakama.
Mwili wa Shukri ulichukuliwa na wananchi na kupelekwa katika msikiti ulioko Mukuru kwa Njenga kwa maombi na hatimaye akazikwa baada ya kufanyiwa upasuaji kubaini kiini cha kifo.
Jibril aliomba washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 21 kuwezesha IPOA kukamilisha uchunguzi.
Zoezi hilo la IPOA korti ilielezwa itajumuisha kuandika taarifa za mashahidi na kupelekwa hospitali kupimwa akili kubaini ikiwa wawili hao wako na utimamu wa akili kabla ya kushtakiwa kwa mauaji.
Washukiwa hao walipinga kusukumwa jela siku 21 wakisema wameshirikiana na wachunguzi wa IPOA.
Akiamuru polisi hao wazuiliwe rumande hakimu alisema wapelelezi wanahitaji kukamilisha zoezi na kuwahoji mashahidi.
Hakimu alisema wawili hao sharti wapelekwe kupimwa ikiwa akili zao ni timamu kuwezesha washtakiwe kwa mauaji.
“Mtazuiliwa kwa siku14 kusaidia polisi kukamilisha uchunguzi,” aliamuru hakimu.
Kesi hiyo itatajwa Januari 26, 2026 kwa maagizo zaidi.