Akili Mali

AKILI MALI: Alijifunza usonara kwa kuangalia wajuzi wengine

Na KALUME KAZUNGU January 13th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

BAYA Mugaza Ndale ni sonara tajika kisiwani Lamu. Mara nyingi unapopita kwenye duka la Slim Silversmith lililoko mtaa wa Mkomani ulioko katikati mwa Mji wa Kale wa Lamu, utampata Bw Mugaza akiwa amejibanza kwenye mojawapo ya kona za duka hilo.

Akishikilia bomba la gesi lililowashwa moto nchani, sonara huyo utampata akiwa ameelekeza fikra zake zote katika kuyaandaa mapambo ya fedha, akianza kwa kuchomelea na kuiyeyusha fedha yenyewe, kuikausha, kuinyosha, kuikombosha hadi kuafikia pambo husika linalohitajika.

Kisha yeye hulifua pambo hilo la fedha, iwe ni pete, keekee, herini, mkufu na kafhalika ilmradi imeremete kabisa.

Anakiri kuienzi kazi hiyo ambayo ameifanya kwa zaidi ya miaka thelathini sasa.

Baada ya kumaliza masomo yake ya darasa la nane kwenye shule ya msingi ya Bedida iliyoko Kaloleni, Kaunti ya Kilifi mnamo mwaka 1991, Bw Mugaza hakuweza kuendeleza masomo yake ya sekondari kutokana na umaskini ulioizonga familia yake.

Badala yake, alijitosa kwenye kazi mbalimbali ili kuyakimu maisha yake.

Alisafiri hadi Mombasa alikobahatika kuajiriwa kama mfagiaji kwenye duka moja la mfuafedha mtaani Kibokoni.

Ni hapo ambapo Bw Mugaza alifaulu kujitwalia ujuzi au usonara kupitia kuwatazama mafundi wakifua fedha na kutengeneza mapambo mbalimbali.

Ujuzi huo ambao hakuusomea darasani ila kupitia kutazama na kuiga jinsi waliobobea walivyoifanya kazi hiyo, ndio ambao leo umemwezesha kuyasukuma maisha yake na yale ya familia yake inayojumuisha mke na watoto wawili.

Baada ya kufanya usonara kwa miaka mingi mjini Mombasa, aliitwa Lamu karibu miaka mitano iliyopita, ambapo aliajiriwa kwenye duka alimo sasa la Slim Silversmith.

“Mimi sijalipa fedha zozote kujiunga na taasisi au chuo kusomea usonara. Ujuzi niliupata kupitia kuwatazama marafiki na wazee waliobobea nyanjani, hivyo nikashika hadi kuwa mweledi kabisa,” akasema Bw Mugaza.

Mapambo anayotengeneza dukani humo huyauza kwa kati ya Sh1,000 na Sh10,000 kulingana na ukubwa, aina ya pambo na fasheni ambayo mteja huagiza.

Wateja wake wengi ni Waswahili wa jamii ya Wabajuni aliowataja kuwa wenye kuthamini mapambo si haba.

Wageni na watalii wa ndani kwa ndani na ng’ambo pia ni miongoni mwa wateja wanaozuru kwa wingi dukani hapo kwani sifa za Bw Mugaza katika kutengeneza mapambo ya fedha zimeenea ndani na nje ya kisiwa cha Lamu.

Anasema mwezi mzuri yeye hakosi kuunda zaidi ya Sh40,000 kupitia ufuaji wa fedha, kutengeneza mapambo na kuyauzia wateja dukani humo.

Pia ni mkufunzi kwa wale wanaomezea mate ujuzi wake.

Mugaza Ndale, 51, akiyeyusha fedha kuunda pete na mapambo mengine katika duka la Slim Silversmith, Mji wa Kale wa Lamu Desemba 7, 2025.
PICHA|KALUME KAZUNGU

Wanaopokezwa maarifa hayo hulipa kati ya Sh4,000 hadi Sh10,000 kwa mwezi kulingana na hali ya mhusika, hivyo kumwezesha Bw Mugaza kuinua kipato chake cha kila mwezi.

“Usonara nauchukulia kuwa kazi sawa na taaluma nyingine yoyote, iwe ni ualimu, udaktari, uuguzi na kadhalika. Mtaji ninaopata hapa umesaidia kuyasukuma maisha na kukimu mahitaji ya familia,” anasema.

Ni kupitia kazi hiyo ambayo imemwezesha kufungua duka lake mwenyewe la kufua na kutengeneza mapambo ya fedha mjini Watamu, Kaunti ya Kilifi.

Watoto wake wawili, mvulana na msichana wako miaka 22 na 21 kwa sasa, ambapo kijana ndiye msimamizi wa tawi la kufua fedha lililoko Watamu.

“Kijana wangu aliipenda sana hii kazi ya kufua fedha na kutengeneza mapambo. Nilimfunza mwenyewe hadi akaimarika kabisa. Baada ya kufungua duka langu Watamu, yeye ndiye meneja pale. Msichana nilimsafirisha kufanya kazi nje ya nchi,” anaeleza.

Miongoni mwa watu anaowakumbuka na kuwaenzi kwa kuchangia ufanisi wa kazi yake ni mwajiri wake wa sasa katika duka la Slim Silversmith, Bw Mubarak Omar Slim ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Mzee Slim niliwahi kufanya kazi na yeye eneo la Kibokini, Mombasa na kisha baadaye tukapoteleana. Baada ya mzee kufariki karibu miaka mitano iliyopita, mtoto wake alinitafuta na kunisihi nikae kwa duka hili kuendeleza biashara ya mzee Slim,” anasema Bw Mugala.

Wengine waliomshika mkono ni Bw Munir Mohamed na nduguye, Bw Swaleh Mohamed, wote akiwahi kutangamana nao na kumfunza usonara eneo hilo hilo la Kibokoni.

Baadhi ya changamoto anazozitaja kukumbana nazo kazini ni kwamba misimu mingine biashara huenda chini, ambapo anaweza kukaa miezi miwili au hata mitatu bila ya wateja kufika kununua au kuweka oda ya mapambo.

Ukosefu wa vifaa vya kujilinda pia umemwacha na makovu, ikiwemo kuchomekachomeka ncha za vidole anapotekeleza kazi hiyo ya kila siku.

Bw Baya Mugaza Ndale alizaliwa Julai 7, mwaka 1975 katika eneo la Rabai, kaunti ya Kilifi. Kwa sasa ana umri wa miaka 51.

Anawashauri vijana kuchangamkia kazi za mikono na kutia bidii kujimudu maishani, wajiajiri badala ya kurandaranda mitaani wakisubiri kuajiriwa maofisini.