Habari za Kaunti

Benki yaonya wanasiasa dhidi ya kupotosha kuhusu uhalalishaji wa ardhi Mavoko

Na STANLEY NGOTHO January 14th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

Benki ya Kenya Commercial (KCB) imewaonya wanasiasa katika Kaunti ya Machakos  dhidi ya kuingiza siasa katika zoezi linaloendelea la kuhalalisha umiliki wa ardhi kaunti ya Mavoko, ikisisitiza kuwa mchakato huo ni wa wazi na wa haki.

Mnamo Jumatatu, Mbunge wa Mavoko, Patrick Makau, aliwashutumu baadhi ya wanasiasa wa eneo hilo akidai wameteka zoezi hilo kwa manufaa yao ya kifedha, hali ambayo imewaumiza wamiliki maskini wanaotarajia kuhalalisha umiliki ardhi hiyo.

“Zoezi la kuhalalisha umiliki wa ardhi lilitekwa na bei za ploti zikapanda hadi Sh2.5 milioni kwa ploti, ili kunufaisha wanasiasa wa eneo hilo. Hatuwezi kuruhusu wanasiasa wabinafsi kama hao kuendelea kushikilia nyadhifa za umma,” alilalamika mbunge huyo.

Mbunge huyo anayejulikana kwa kauli kali alidai kuwa wamiliki wengi wa wanaoishi kwenye ardhi hiyo hawawezi kumudu bei hizo zilizopandishwa na mawakala wa KCB.

“Wengi wao wako hatarini kufurushwa baada ya kuishi katika ardhi hii kwa miaka mingi. Haki na utu viko wapi?” alihoji.

Hata hivyo, katika taarifa iliyotolewa Jumanne, KCB,  kupitia Meneja wa mradi, Antony Njuguna, iliwashutumu wanasiasa kwa kusambaza habari za kupotosha na kuwachochea wamiliki wa ploti, hali iliyosababisha taharuki na mkanganyiko usio wa lazima kuhusu zoezi hilo.

Njuguna alisisitiza kuwa ardhi hiyo inauzwa na kwamba hakuna ploti zilizotengwa kwa manufaa ya mwanasiasa yeyote. Aliongeza kuwa bei ni sawa kwa wanunuzi wote na masharti ya malipo ni nafuu kwa kila mtu.

“Kama wakala wa KCB, tulianza zoezi hili mwaka jana na kundi la kwanza la wamiliki litapokea hati zao za umiliki kwa wakati unaofaa. Wamiliki wasipotoshwe na wanasiasa. Mchakato huu ni halali,” alisema Njuguna. “Ardhi hii inamilikiwa na KCB. Ni biashara ya kawaida ya mali isiyohamishika kwa wanunuzi wote. Siasa hazina nafasi katika mradi wa Simba City.”

Kati ya mwaka 2021 na 2022, kampuni kubwa ya serikali ya kutengeneza simiti (EAPC) ilikabidhi ekari 1,167 za ardhi yake Athi River kama sehemu ya mpango wa kulipa deni la jumla la Sh6.8 bilioni iliyokuwa ilidaiwa  na KCB.

Mwaka jana, KCB ilianza zoezi la kuhalalisha umiliki wa ardhi hiyo kwa kuwapa kipaumbele wamiliki waliokuwa wamejenga hapo kulipia ploti zao kabla ya ardhi hiyo kufunguliwa kuuzwa kwa umma.

Waliokuwa wameishi katika ardhi hiyo walitakiwa kujisajili na KCB na kulipa amana baada ya zoezi la upimaji. Gharama ya kila ploti ilitegemea ukubwa wake.

Kwa sasa, takribani asilimia 80 ya ardhi hiyo imeendelezwa, ikiwa na nyumba za kifahari, makanisa, shule na mikahawa ya hadhi ya juu.