Wamatangi alaumu siasa mali ya mamilioni ikibomolewa Nairobi
GAVANA wa Kiambu Kimani Wamatangi ametaja ubomoaji wa biashara zake zilizo karibu na Uwanja wa Nyayo kama mateso ya kisiasa, akisema amekuwa akikodisha ardhi hiyo kutoka Shirika la Reli Kenya kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Biashara hizo, zilizoko kando ya Barabara ya Douglas Wakiihiru karibu na Barabara ya Lang’ata, nyuma ya Uwanja wa Nyayo, zilibomolewa Jumanne usiku, ikiwa ni mara ya pili zoezi kama hilo kufanyika katika eneo hilo.
Chini ya ulinzi wa polisi waliokuwa na silaha kali, tingatinga zilivamia eneo hilo na kubomoa majengo mawili ya muda, huku mali nyingine katika eneo hilo, ikiwemo magari, ikiharibiwa.
Jumatano, Gavana wa Wamatangi alivunja kimya chake kufuatia kubomolewa kwa biashara hizo akidai hatua hiyo imelenga kumhangaisha kisiasa na kumlazimisha ajiondoe kwenye kinyang’anyiro cha ugavana wa 2027.
Akizungumza alipotembelea eneo lililobomolewa huku kukiwa na ulinzi mkali wa polisi, Wamatangi alisisitiza kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa biashara hizo.
Gavana huyo alitaja ubomoaji huo kama mateso ya kisiasa, akidai ni sehemu ya juhudi za serikali kumhangaisha na kumzuia kutekeleza wajibu wake kwa wananchi wa Kiambu.
“Nilianzia hapa nikiwa mvulana mdogo nikiuza chai na mandazi, nikajijenga polepole hadi nikaanzisha biashara iliyokuwapo hapa. Kilichotokea ni cha kisiasa kabisa, kinalenga kuninyamazisha na kunitisha,” alisema Wamatangi.
Aliahidi kuendelea na azma yake ya kisiasa licha ya tukio hilo, akisema: “Kama unataka kuwa Gavana wa Kiambu, unapaswa kuwafuata wananchi, si kutumia vitisho. Sitatishwa, na nitawania ugavana bila woga wala upendeleo.”
Walioshuhudia walisema polisi waliokuwa eneo hilo walifyatua risasi hewani na kutumia vitoa machozi kusimamia zoezi hilo na kuwatisha waliokuwapo wakati wa ubomoaji.
Hata hivyo, Wamatangi alisema hatalipiza kisasi, bali ataacha suala hilo mikononi mwa Mungu huku akisisitiza kuwa atafuata njia za kisheria na amani.
Alifichua pia kuwa ana mkataba wa upangaji wa ardhi wa miaka 65 kutoka Shirika la Reli Kenya na amekuwa akilipa kodi kila mwezi bila kukosa, hivyo hakukuwa na suala lolote la kukiuka masharti.
Gavana huyo aliongeza kuwa licha ya kupata taarifa za mapema kuhusu ubomoaji huo, hakuweza kufika eneo hilo mapema alfajiri kutokana na taarifa za ufyatuaji wa risasi. Alisema alihofia usalama wake, akihisi kuwa risasi zilizokuwa zikifyatuliwa huenda zililenga maisha yake.
Kuhusu iwapo alipewa notisi rasmi kabla ya ubomoaji, Wamatangi alisisitiza kuwa yeye wala timu yake hawakuwahi kupokea hati yoyote.
“Nina uhakika kabisa kwamba hakukuwa hata notisi ya siku moja. Kama kulikuwa na notisi, waionyeshe,” alitoa changamoto.
“Nilianza kufanya kazi hapa mwaka 1994, nikiosha magari na baadaye nikaanza biashara ya kuuza magari. Nimejilea katika eneo hili, nikiwa na mkataba wa upangaji ninaolipa kila mwezi. Kile kilichotokea leo ni siasa tupu,” aliongeza.
Ubomoaji huo ulilenga biashara na mali ya thamani ya mamilioni ya pesa ili kupisha mradi wa miundombinu unaotarajiwa.
Miongoni mwa mali iliyobomolewa kando ya Barabara ya Douglas Wakiihiru, nyuma ya Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo, ni pamoja na viwanja vya kuuza magari, karakana ya kuosha magari, mkahawa na biashara nyingine.
Shirika la Reli limetoa notisi iliyoarifu wenye biashara zilizo eneo hilo kuwa zingebomolewa iwapo hawangehama ndani ya siku saba kuanzia Novemba 1, 2023.
Wamatangi alisema alikuwa ameenda kortini baada ya vitisho vya maneno kutoka kwa baadhi ya maafisa kwamba mali hiyo ingebomolewa.