Makala

Ukame Kaskazini mwa Kenya wagutusha kuhusu ahadi ya Ruto ya mabwawa 200

Na MANASE OTSIALO January 16th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HOFU imetanda Kaskazini mwa Kenya kutokana na ukame mkali unaokumba kaunti za eneo hilo na kuhatarisha maisha na riziki za wakazi.

Kaunti ya Mandera, kwa mfano, imeanza kushuhudia vifo vya mifugo, huku ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Msalaba Mwekundu nchini ikionyesha kuwa hali inazidi kuwa mbaya katika maeneo ya Mandera Kaskazini, Banisa na Mandera Magharibi.

Wafugaji wengi katika kaunti hiyo wanakadiria hasara kubwa baada ya mifugo yao kufa kutokana na ukosefu wa malisho na maji.

Mohamed Hussein, mkazi wa eneo hilo, anasema amepoteza idadi kubwa ya mbuzi kutokana na ukame huo, huku wale wachache waliobaki wakikabiliwa na hatari ya kufa pia.

“Nilikuwa na takriban mbuzi 200 lakini sasa wamebaki 15 pekee. Wanakufa kila siku kwa sababu ya ukosefu wa malisho na maji,” alisema.

Hali si tofauti katika eneo la Banisa ambako vyanzo vikuu vya maji vimekauka, na kulazimisha wakazi kutegemea maji yanayoletwa kwa malori.

“Vyanzo vyetu vikuu vya maji mjini vimekauka. Mji umekuwa kavu na kupata maji sasa ni changamoto kubwa,” alisema mkazi mmoja.

Kutokana na hali hiyo, Baraza la Magavana (CoG) limeitisha msaada wa dharura na kuitaka serikali kuingilia kati mara moja.

Akizungumza wakati wa Jukwaa la Washirika wa Maendeleo la 2026 lililofanyika katika Makazi ya Naibu Rais jijini Nairobi, Mwenyekiti wa CoG, Ahmed Abdullahi, alisema hali ya ukame inaendelea kuwa mbaya.

Gavana huyo wa Wajir alihusisha hali hiyo na misimu mitatu mfululizo ya uhaba wa mvua.

“Kaunti kame zinaendelea kukumbwa na hali mbaya ya ukame baada ya mvua kukosa kunyesha. Katika kaunti nyingi, mvua fupi kati ya Oktoba na Desemba haikunyesha, hali iliyosababisha uhaba mkubwa wa maji na kuongeza shinikizo kwa binadamu,” alisema.

Alisema athari za ukame huo zinajitokeza pia katika maeneo mengine ya nchi kupitia kupanda kwa bei ya vyakula, uhaba wa maji na kuvurugika kwa uchumi.

“Vyanzo vingi vya maji vimekauka katika kaunti nyingi na uzalishaji wa mazao umeathirika, jambo lililosababisha ongezeko la bei ya vyakula sokoni,” aliongeza.

Bw Abdullahi alisema akina mama wajawazito, kina mama wanaonyonyesha na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ndio wanaoathirika zaidi kutokana na ukosefu wa lishe bora.

“Mifugo inaangamia kwa sababu ya ukame na bei yake sokoni imeshuka pakubwa kiasi kwamba kwa Sh500 tu unaweza kununua kondoo,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa CoG alisema kaunti zimeunda Kamati za Kukabiliana na Ukame na Majanga, pamoja na kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema na uratibu.

Alisema hatua kama usafirishaji wa maji kwa malori, ukarabati wa visima na ulinzi wa vyanzo muhimu vya maji zinaendelea kutekelezwa.

“Baadhi ya kaunti zinatoa chakula na huduma za ulinzi wa kijamii ikiwemo mipango ya kutoa pesa taslimu ili kusaidia maisha ya wakazi,” alisema.

Aliitaka Serikali ya Kitaifa kusaidia serikali za kaunti katika juhudi za kuzuia janga kubwa zaidi kwa kutoa chakula kwa binadamu na malisho kwa mifugo.

“Tunahitaji chakula, kuongezwa kwa upatikanaji wa maji, magari zaidi ya kubeba maji na mpango wa kununua mifugo kutoka kwa wafugaji,” alisema.

Huku Baraza la Magavana likitaka serikali kutangaza hali ya dharura ya ukame, Naibu Rais Kithure Kindiki alitangaza kutengwa kwa Sh6 bilioni kukabiliana na ukame huo.

Akizungumza katika jukwaa hilo hilo, Prof Kindiki aliwahakikishia Wakenya kuwa serikali iko tayari kukabiliana na hali hiyo na kwamba hatua zinazofaa zimechukuliwa.

Naibu Rais aliwataka wananchi wawe watulivu, akisema fedha hizo tayari zimetengwa kusaidia juhudi za kukabiliana na ukame na kuwaomba washirika wa maendeleo kuongeza mchango wao.

“Serikali imejiandaa kuhakikisha tunatoa chakula cha kutosha kwa wote walioathirika na pia kuokoa mifugo yao. Hakutakuwa na hofu nchini,” alisema.

Alielezea ukame wa sasa kama athari ya mabadiliko ya tabianchi itakayodumu kwa muda mfupi.