Habari za Kaunti

Afisa aua mwenzake na kujimaliza kwa risasi katika mzozo wa ‘mbuzi wa Krismasi’

January 16th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

AFISA wa polisi na mwingine wa Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori nchini (KWS), walipoteza maisha yao Jumatano kwenye mzozo kuhusu mbuzi wa msimu wa sherehe za Desemba, uliosababisha ufyatuaji risasi.

Kisa hicho kilichotokea katika Kaunti-ndogo ya Kinango, Kaunti ya Kwale, kilisababisha pia watu wengine wawili kujeruhiwa, akiwemo raia mmoja.

Kwa mujibu wa polisi, askari wa KWS John Ndichu kutoka kambi ya KWS ya Kilibasi aliwafyatulia risasi maafisa wa polisi na raia mmoja, kisha baadaye akajipiga risasi chini ya kidevu na kufariki papo hapo.

Afisa wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Kilibasi, Stanley Karithi, alipigwa risasi na kufariki, huku mwenzake Aftin Farah Ali akijeruhiwa vibaya.

Tukio hilo lilitokea Jumatano alasiri katika barabara ya Nyango–Kilibasi eneo la Vigurunganimwendo wa saa kumi na mbili jioni.

Maafisa hao wawili wa polisi walikuwa wamesimamisha pikipiki iliyokuwa imebeba makaa wakati walipokutana na Ndichu na askari mwenzake wa KWS Eric Mugambi, ambao pia walikuwa kwenye pikipiki.

Katika mazungumzo yao, Bw Karithi alimhoji Ndichu kuhusu mbuzi wawili wanaodaiwa kupewa kwake na mfugaji wakati wa msimu wa sikukuu, ambao walikusudiwa kwa maafisa wa polisi lakini hawakuwahi kufikishwa.

Hali iliharibika kwa haraka, huku Ndichu akifyatua risasi kutoka kwenye bunduki yake.

“Ndichu alikasirika na kuanza kufyatua risasi kutoka kwenye bunduki yake, akimpiga risasi polisi Stanley Karithi mara nne kifuani na kumuua papo hapo, kabla ya kumpiga risasi polisi Aftin Farah Ali na mwendesha pikipiki,” ripoti ya polisi ilisema.

Bw Ali alipigwa risasi upande wa kulia ubavuni na kupata majeraha mabaya, kisha akakimbizwa hadi Hospitali ya Voi.

Mwendesha pikipiki aliyetambuliwa kama Salim Mwandoro, naye pia alipigwa risasi upande wa kulia wa mbavu, akapata majeraha mabaya na kukimbizwa hadi Hospitali ya Mariakani kwa matibabu.

Maafisa wakuu wa usalama, wakiwemo Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kinango, maafisa kutoka Vigurungani na Mackinnon Road, pamoja na wapelelezi kutoka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), walifika katika eneo la tukio kuanzisha uchunguzi.

Polisi walisema walipata silaha mbili ambazo zilikuwa za maafisa hao pamoja na risasi katika eneo la tukio.

“Tukio hili bado linaendelea kuchunguzwa na faili ya uchunguzi wa kifo imefunguliwa,” ripoti hiyo ilisema, ikiongeza kuwa uchunguzi unashughulikiwa na DCI wa Kinango.