Jamvi La Siasa

Musalia, Weta waumwa kichwa ushawishi wao Magharibi ukipingwa na wanasiasa wachanga

Na ERIC MATARA January 16th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

KWA takriban miongo miwili, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula wamekuwa wakiongoza siasa za Magharibi mwa Kenya, wakiongoza katika kubuni ushirikiano katika ngazi ya kitaifa na kutoa mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo.

Wote wawili, wanaoonekana kama vigogo wa kisiasa wenye ushawishi mkubwa katika jamii ya Waluya, wamejipa heshima kutokana na uzoefu wao, ujuzi wa kisiasa na kuunda sera za eneo na taifa kwa jumla.

Mudavadi na Wetang’ula walichukua uongozi wa siasa za Magharibi baada ya kifo cha aliyekuwa makamu wa rais Michael Wamalwa mwaka wa 2003, na tangu wakati huo wameonekana kama viongozi wa kiasili wa Magharibi mwa Kenya.

Mudavadi, aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka wa 1989, amewahi kushikilia nyadhifa kadhaa za juu serikalini ikiwemo Makamu wa Rais, Waziri wa Fedha, na Kiongozi wa Chama cha ANC, ambacho alianzisha, akijipa sifa ya kiongozi wa wastani na mwingi wa uzoefu.

Bw Wetang’ula, kiongozi wa chama cha Ford Kenya, naye ni mwanasiasa aliyebobea, na kupitia ushirikiano wake na Mudavadi, amehakikisha eneo la Magharibi lina usemi katika siasa za kitaifa.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, wawili hao walipata nyadhifa muhimu katika serikali ya Kenya Kwanza, baada ya kuungana na Rais William Ruto, na tangu wakati huo wamekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za eneo na taifa.

Hata hivyo, miezi ya hivi karibuni, ushawishi wao Magharibi mwa Kenya umeanza kupingwa na wanasiasa wachanga wenye nguvu mpya na uhusiano wa mashinani na wananchi.

Viongozi kama Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Seneta Edwin Sifuna (Nairobi), Godfrey Osotsi (Vihiga), na Mbunge wa Saboti Caleb Amisi wamekuwa mwiba kwa Mudavadi na Wetang’ula, wakipinga mtindo wao wa uongozi na kudai kwamba wawili hao hawajachangia maendeleo katika eneo hilo.

Katika mahojiano na Taifa Leo jana, Gavana Natembeya alisema kuwa ana malengo ya kuunganisha Magharibi mwa Kenya na wananchi kwa ujumla kabla ya uchaguzi wa 2027, bila kusema wazi kama anamezea mate wadhifa wa kitaifa.

“Viongozi hawa wameshindwa kimsingi katika uongozi wa Magharibi na kitaifa kwa jumla. Lengo langu ni kuunganisha Magharibi mwa Kenya na Wakenya kwa jumla kuelekea uchaguzi wa 2027. Hakuna maendeleo ya maana, hakuna ajira mpya wameleta katika eneo letu,” alisema Natembeya.

Aliongeza kuwa ushawishi wa Mudavadi na Wetang’ula unatokana na Rais Ruto wanayemkumbatia ili kuepuka hatari ya kupoteza kisiasa.

Alisisitiza kuwa Magharibi haina kiongozi wa kisiasa anayeweza kuzungumza kwa niaba ya jamii katika meza ya kitaifa, na kwamba yeye yuko tayari kutoa uongozi unaohitajika.

Hata hivyo, msemaji wa muda mrefu wa Mudavadi, Prof Kibisu Kabatesi, alihoji kwamba wawili hao bado ni viongozi wa Waluhya.

“Mudavadi na Wetang’ula bado wana heshima na ushawishi mkubwa. Mudavadi hivi karibuni alishinda uchaguzi mdogo wa eneobunge la Malava, kuonyesha kuwa bado ana nguvu Magharibi mwa Kenya,” alisema Kabatesi. Aliongeza kuwa viongozi vijana wanapaswa kuheshimu vigogo na kujifunza kuwa uongozi wa kisiasa ni mchakato unaohitaji uvumilivu, ushauri na mshikamano.

Hata hivyo, wachambuzi wa kisiasa wanasema kuwa ushawishi wa Mudavadi na Wetang’ula unafifia polepole, jambo linalowatia wasiwasi washauri wao huku uchaguzi wa mwaka ujao ukikaribia.

Mchambuzi wa siasa za eneo hilo Bw Peter Wafula alisema wananchi na viongozi wanajiuliza maswali na kuanza kusikiliza sauti mbadala na kwamba “wawili hao wako katika hatari ya kupoteza umaarufu”.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Prof Tom Nyamache, sauti za vijana na wanasiasa wachanga hazipaswi kupuuzwa.

“Mudavadi na Wetang’ula hawawezi kustawi bila kuzingatia changamoto hizi. Kabla ya 2027, ushawishi wao unaweza kupungua.”

Gavana Natembeya amekuwa mstari wa mbele kuunganisha jamii ya Waluya katika kaunti za Vihiga, Bungoma, Busia, Kakamega na Trans Nzoia, na anashikilia nafasi ya kiongozi mbadala, huku utafiti wa hivi majuzi wa Infotrak ukimpa asilimia 36 ya umaarufu ndani ya jamii ya Waluya, mbele ya Mudavadi (asilimia 18) na Wetang’ula (asilimia 14).

Waziri Wycliffe Oparanya anafuatia kwa asilimia nane.

Wanaohoji ushawishi wa Mudavadi na Wetang’ula wanasisitiza kwamba muda wao wa kuongoza eneo umepita na wanapaswa kupisha viongozi vijana.