Makala

Nabii Nabwera ataka Savula amlipe Sh100m kwa dai alimchafulia jina

Na RICHARD MUNGUTI January 15th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Lugari, Nabii Daraja Nabwera amemshtaki Naibu Gavana wa Kaunti ya Kakamega, Ayub Savula akitaka amlipe fidia ya zaidi ya Sh100 milioni kwa kumharibia sifa na jina kwamba anaugua maradhi mabaya.

Katika kesi yake, Bw Nabwera ameomba Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi imwamuru Bw Savula amuombe msamaha na kufutilia mbali matamshi hayo ya kumkejeli, kumshusha hadhi na kumfedhehesha.

Kupitia wakili Danstan Omari mbunge huyo amedai mwanasiasa huyo alimkejeli alipowahutubia waombolezaji mnamo Novemba 25, 2025 wakati wa mazishi ya mwalimu mkuu aliyekufa kwa njia tatanishi.

Bw Nabwera anaeleza katika ushahidi aliowasilisha mahakamani kwamba Bw Savula alimkaripia na kutoa matamshi ya uwongo kwamba anaugua maradhi ambayo hatuwezi kuchapisha.

Kuthibitisha kwamba yeye ni mzima kama kigongo, Bw Nabwera ameomba mahakama itoe maagizo afanyiwe utafiti wa kiafya katika Uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Kasarani ama bustani ya Uhuru Park.

Aliomba hafla hiyo ya kupimwa kwake iangaziwe na vyombo vyote vya habari.

Bw Nabwera ameiomba Mahakama imzime mshtakiwa (Savula) ama maajenti wake kisiasa kumharibia jina au kushusha hadhi yake hadharani kabla ya kesi hiyo aliyomshtaki kusikizwa na kuamuliwa.

Pia mlalamishi (Nabwera) ameomba korti itoe maagizo yale inayoona yanafaa yatulize uhusiano mbaya unaotokota baina ya wawili hao.