Ruto adai Uhuru anafadhili uasi ODM
RAIS William Ruto anasemekana kumlaumu mtangulizi wake, Rais Uhuru Kenyatta, kwa kufadhili baadhi ya viongozi wa ODM kupinga serikali jumuishi na kusababisha mgawanyiko katika chama hicho.
Akizungumza alipokutana na madiwani wa Kaunti ya Siaya Januari 10 katika Ikulu Ndogo ya Eldoret, Rais alimtaja hasa Gavana wa Siaya, James Orengo, akisema baadhi ya viongozi wanaopinga mipango ya kitaifa wanashawishiwa na Bw Kenyatta.
“Rais alisema Orengo sasa ni mwanasiasa aliyekomaa na hapaswi kushawishiwa na siasa au fedha za Uhuru Kenyatta. Alisema kama Orengo ana shida yoyote, basi awasiliane na Rais moja kwa moja,” alisema MCA wa Alego ya Kati, David Ragen.
Ziara hiyo ilihudhuriwa na madiwani 41 kati ya 42 wa Kaunti ya Siaya, wakiongozwa na Spika wao George Okode. Gavana Orengo, Naibu wake William Oduol na wabunge wa kaunti hiyo hawakuhudhuria. Hata hivyo, Waziri wa Kawi na Petroli, Opiyo Wandayi, na Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Raymond Omollo, walihudhuria.
Rais Ruto aliwapa madiwani maelezo ya kina kuhusu mpango wake wa kitaifa na umuhimu wa kushirikiana na kaunti kwa maendeleo. Alisisitiza kuwa Serikali Jumuishi ina ajenda madhubuti kwa taifa, na kuwa mipango yote ya kitaifa itatekelezwa kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya wananchi.
“Nilikutana na madiwani wa Bunge la Kaunti ya Siaya wakiongozwa na Spika George Okode katika Ikulu Ndogo ya Eldoret. Tulikubaliana kuharakisha miradi inayoendelea na kusukuma mbele miradi iliyopangwa, ili maendeleo yawafikie wananchi moja kwa moja,” alisema Rais Ruto.
Hata hivyo, mjadala katika mkutano huo ulikuwa pia na mada ya kisiasa, hasa kuhusiana na Gavana Orengo. Spika Okode alisema mkutano huo ulikuwa wa kufuatilia ahadi za maendeleo ambazo Rais alikuwa ametoa awali kwa viongozi wa Siaya katika Ikulu ya Nairobi.
“Tulikuwa tukifuatilia utekelezaji wa miradi ambayo Rais alituahidi. Tulitaka kujua ni yapi yametekelezwa kutoka kwa makubaliano tuliyowasilisha kwake,” alisema Okode.
Alikanusha madai kwamba mkutano huo ulimtenga Gavana Orengo, akisema ulikuwa mahsusi kwa Bunge la Kaunti na Rais, ndiyo maana gavana, naibu wake na wabunge hawakuhudhuria. Aliongeza kuwa salamu za gavana ziliwasilishwa kwa Rais, akisisitiza kuwa Orengo anaunga mkono ushirikiano wa kisheria kati ya serikali ya kitaifa na kaunti.
Rais aliwataka madiwani kumwambia gavana kuwa asishawishiwe na pesa au siasa za mtu yeyote, bali awe wazi na kushirikiana moja kwa moja na serikali. Bw Ragen, alisema Rais aliwatuma wakamwambie gavana kuwa wana historia ndefu pamoja na wanapaswa kusuluhisha tofauti zao kwa mazungumzo ya moja kwa moja.
Dkt Omollo pia aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wanaweza kuwa wanamkosoa Rais hadharani mchana lakini humtafuta faraghani usiku, akisisitiza umuhimu wa uwazi na uaminifu katika siasa. Hata hivyo, madiwani walikanusha madai yoyote ya njama za kumng’atua gavana. “Hakukuwa na mazungumzo ya kumuondoa gavana. Orengo hawezi kung’atuliwa, hakuna mtu anayeweza kujaribu,” alisema MCA wa West Gem, Susan Nyamawira.
Katika mkutano uliochukua saa nne, mada ya siasa jumuishi, maendeleo ya Siaya, uchaguzi wa 2027, na ajenda ya kitaifa yalijadiliwa. Madiwani pia waliwasilisha hoja zao kuhusu maslahi yao ikiwemo mfumo wa ununuzi wa kielektroniki, mishahara, pensheni za madiwani na bajeti za bursary za wadi.
Rais pia alisimulia historia yake ya kisiasa na Raila Odinga, akisisitiza kuwa makubaliano ya serikali jumuishi yalifungua njia ya kurekebisha dhuluma za kihistoria dhidi ya Nyanza.