Habari

Aliyeng’olewa jino vibaya na daktari bandia afariki

Na MERCY CHELANGAT January 16th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KILICHOKUWA ziara ya kawaida ya kutuliza maumivu ya jino kiligeuka kuwa mkasa mkazi wa Kawangware, Amos Isoka, alipofariki Jumatano usiku katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) baada ya kung’olewa jino vibaya na mtu asiye na leseni.

Mke wake, Vivian Nanjala, alithibitisha kifo hicho akisema juhudi za madaktari kumuokoa mumewe hazikufaulu.

“Mume wangu amefariki. Alikufa saa tano usiku wa Jumatano. Tumevunjika moyo sana,” alisema Nanjala.

Isoka, mzaliwa wa kwanza katika familia ya watoto wanne, alikuja Nairobi kutafuta riziki. Kulingana na Nanjala, ndoto yake ilikuwa kujiwekea akiba ili kununua ardhi ya kumjengea mamake makazi. Ndoto hiyo sasa imekatizwa na kifo chake.

“Mama yake anaelekea mashambani kuanza maandalizi ya mazishi huku mimi nikirejea hospitalini kuthibitisha bili na kuanza taratibu za kuhifadhi mwili. Aliyesababisha haya bado hajakamatwa,” alisema.

Siku ya Mwaka Mpya, Isoka alitembelea kituo kimoja cha afya Kawangware kinachojulikana kama Life Clinic akilalamikia maumivu ya taya. Alitozwa Sh1,000 kung’olewa jino na mtu aliyekuwa akijifanya mtaalamu. Ndani ya saa 24, hali yake ilidorora kwa kasi, akavimba shingo, ulimi na kifua.

Madaktari katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta (KNH) waligundua alikuwa na ugonjwa hatari unaojulikana kama Ludwig’s angina, maambukizi makali yanayoenea chini ya mdomo na yanayweza kuziba njia ya hewa. Licha ya kufanyiwa upasuaji mkubwa mara mbili na kutibiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, Isoka alipata matatizo makubwa ya kupumua na kufariki Jumatano jioni.

Katika taarifa, Rais wa Chama cha Madaktari wa Meno Kenya (KDA), Dkt Kahura Mundia, alilaani mfumo wa udhibiti ulioruhusu mkasa huo. Alisema tukio hilo linaonyesha hatari kubwa ya watu wasiohitimu wanaojifanya wataalamu wa afya.

Dkt Mundia alisisitiza kuwa kung’oa jino si jambo dogo na likifanywa na watu wasiohitimu huweza kusababisha maambukizi makali, sumu mwilini, kuziba njia ya hewa, ulemavu wa kudumu au kifo. Alipongeza Baraza la Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDC) kwa kufunga kliniki hiyo haramu, lakini akasema kuchukua hatua baada ya madhara hakutoshia.

KDA imetoa wito wa ushirikiano kati ya mashirika husika na kuongezwa kwa rasilmali ili kukomesha matapeli katika sekta ya afya. KMPDC imewahimiza wananchi kuthibitisha wahudumu kabla ya kutibiwa.