Ruto arudi Nyeri kubomoa Gachagua Mlima Kenya
Rais William Ruto anatarajiwa leo kuhutubia zaidi ya viongozi 18,000 wa mashinani katika Kaunti ya Nyeri katika Ikulu ya Sagana, hatua inayotafsiriwa kama juhudi za kuimarisha na kurejesha uungwaji mkono eneo la Mlima Kenya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Miongoni mwa watakaohudhuria mkutano huo ni maafisa 11,480 waliochaguliwa wiki jana kupitia uchaguzi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) uliofanyika katika vituo 574 vya kupigia kura kote Nyeri. Ujumbe huo pia unajumuisha wabunge, wawakilishi wa wadi (MCAs) na wakazi takriban 7,000, wakiwemo viongozi wa maoni, viongozi wa kidini na wazee, viongozi wa kijamii pamoja na wanachama wa makundi mbalimbali ya kijamii.
Mbunge wa Mathira, Bw Eric Wamumbi, alisema mkutano huo ni wa kuendeleza ziara ya Rais katika kaunti ya Nyeri Jumapili na Jumatatu iliyopita, ambapo alihudhuria ibada katika kanisa eneo la Othaya na kuzindua mpango wa vijana wa Nyota Nyeri, Nyandarua, Murang’a na Kirinyaga.
Bw Wamumbi alisema Rais alivutiwa na mapokezi aliyopata kutoka kwa wakazi wa Nyeri, na akaongeza kuwa katika mkutano wa leo, Dkt Ruto atawapa viongozi hao taarifa kuhusu hatua ambazo serikali yake imepiga katika kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi wa 2022.
“Rais atazungumzia miradi ya barabara inayoendelea katika eneo hili. Ataeleza yale ambayo serikali imefanya katika sekta ya kilimo, ambao ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa eneo hili, pamoja na masuala mengine ya maendeleo,” alisema Bw Wamumbi katika mahojiano ya simu usiku wa Ijumaa.
Aliongeza kuwa Rais pia ataeleza mipango ya serikali kuhusu maendeleo ya maji, elimu, ujenzi wa barabara na miradi mingine, pamoja na ajenda zake kwa kipindi kilichosalia cha muhula wake kabla ya uchaguzi ujao.
Rais Ruto anategemea viongozi hawa wa mashinani wa UDA kufufua uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya ambao umeendelea kudidimia tangu kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kupitia hoja ya kutimuliwa mwezi Oktoba 2024.
Baada ya kuondolewa kwake, Bw Gachagua alimshutumu Rais kwa usaliti na kuanza kampeni za kudhoofisha uungwaji mkono wake katika eneo ambalo lilimpa kura nyingi zaidi katika uchaguzi wa 2022, ambapo asilimia 87 ya kura zake zilitoka Mlima Kenya. Aliungana na viongozi wengine wa upinzani katika harakati za kuhakikisha Rais Ruto anahudumu kwa muhula mmoja pekee.
Ili kukabiliana na shinikizo hilo, Rais alimtuma Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kuongoza jitihada za kisiasa katika Mlima Kenya. Prof Kindiki aliongoza kikosi cha wanasiasa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Mbeere North uliofanyika Novemba 27, 2025, ambapo UDA ilishinda, hatua iliyotajwa kama ishara ya kurejea kwa nguvu kwa chama hicho.
Bw Wamumbi alisisitiza kuwa UDA haijapoteza uungwaji mkono katika eneo hilo kama inavyodaiwa, akisema wakazi wa Mlima Kenya wametambua kuwa upinzani hauna ajenda mbadala ya kuwapa.
“Hawa ni wale wale waliompigia kura kwa wingi Rais Ruto mwaka wa 2022 na hawajabadilika. Wakati wa ziara yake wiki jana, Rais alikagua miradi mbalimbali. Sote tuliona umati wa watu uliomkaribisha. Mwelekeo unabadilika na tunaendelea kurejesha uungwaji mkono wake,” alisema.
Aliongeza kuwa Rais alipokelewa vyema hasa katika mji wa Karatina, eneo analotoka Bw Gachagua, ambapo wakazi walithibitisha kumuunga mkono kwa muhula wa pili.
“Bw Gachagua amepoteza ushawishi kwa sababu amekuwa akichochea watu badala ya kuleta suluhu,” alisema.
Katika Karatina, Rais alizindua soko lililojengwa kwa kipindi cha miezi minane, akakagua ujenzi wa barabara ya Kenol–Marua ambayo imekamilika kwa asilimia 95, na kutathmini maendeleo ya mradi wa nyumba za gharama nafuu. “Hii ni miradi halisi ambayo wananchi wanaweza kuona, si maneno matupu,” aliongeza Bw Wamumbi.
Wakati wa ziara yake Januari 11 na 12, Rais aliwahakikishia wakazi wa Mlima Kenya kuwa hatawaacha, akisema alipata urais kutokana na kura zao nyingi. Pia alipuuza madai ya Bw Gachagua kuwa ndiye aliyemtambulisha Mlima Kenya, akisema alijijengea uungwaji mkono kwa zaidi ya miaka 20, hasa alipokuwa Naibu Rais chini ya Rais Uhuru Kenyatta.
Hata hivyo, viongozi wa upinzani wamepuuzilia mbali juhudi za Rais kuwarai wakazi wa Mlima Kenya, wakisema hakuna kiwango cha ushawishi kitakachobadilisha msimamo wa wakazi wa eneo hilo.
Mbunge wa Mukurweini, Bw John Kaguchia, alisema wakazi wanahongwa kwa pesa ili kuonyesha uungwaji mkono bandia. “Mlima Kenya tayari umeamua. Hakuna kiwango cha kuwarai kitakachobadilisha msimamo wao,” alisema Bw Kaguchia, mshirika wa karibu wa Bw Gachagua.
Mwenyekiti wa chama cha Devolution Empowerment Party (DEP), Bw Titus Ntuchiu, alisema serikali ya Kenya Kwanza imeshindwa kutekeleza ahadi zake kwa wakazi wa Mlima Kenya na nchi kwa jumla.
“Wakenya wanahisi uzito wa uongozi mbaya, ushuru wa kupindukia na gharama ya juu ya maisha. Wanatafuta uongozi unaojali maslahi yao na unaoweza kutekeleza zaidi ya ahadi,” alisema Bw Ntuchiu, ambaye amedhamiria kumuondoa mbunge wa Tigania West wa UDA, Dkt John Mutunga, katika uchaguzi ujao.