Habari za Kitaifa

Wakenya mitandaoni wamshambulia Ruto kwa kumpongeza Museveni

Na FATUMA BARIKI January 18th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

WAKENYA watumiaji mitandao wamekita kambi katika chapisho la Rais William Ruto la kumsifia Rais Yoweri Museveni, 81, kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Januari 15.

Watumiaji mitandao walieleza kushangazwa na pongezi hizo wakisema kulikuwa na kila dalili kwamba uchaguzi mkuu wa Uganda haukuwa huru wala wenye haki na kwamba uligubikwa na dhuluma na vitisho dhidi ya mpinzani wake mkuu, kiongozi mchanga Bobi Wine, 43.

“Baada ya kutangazwa rasmi kwamba umechaguliwa tena kwa muhula mwingine, nakupa pongeza kwa niaba ya serikali na niaba ya Wakenya,” ikasema barua aliyoweka kwenye chapisho lake kwenye X.

SOMA Chapisho la Ruto likipongeza ushindi wa Museveni

Wengi haswa walikejeli aya ya pili ya barua hiyo iliyosema kwamba ushindi wa Bw Museveni ulikuwa usiopingika na kwamba ulikuwa idhibati ya mapenzi ya dhati ya raia wa Uganda kwa chama chake NRM.

“Unawezaje kupongeza Museveni baada ya uchaguzi ambao intaneti ilizimwa, jeshi kumwagwa barabarani, viongozi wa upinzani kukamatwa na wananchi wa kawaida kupigwa kwa kuhudhuria mikutano ya kampeni za Upinzani,” mtumiaji mtandao kwa jina Political Analyst akauliza.

Mwingine, kwa jina Jefahh, akaandika: “Waafrika wenzetu, sisi kama Wakenya hatukubaliani na kile alichosema Rais Ruto. Mtazamo wake ni wa kibinafsi na hausimamii kile mamilioni ya Wakenya wanafikiria. Tunasimama na raia wa Uganda kusema kwamba hakukuwa na uchaguzi.”