Siasa

Winnie apinga Oburu, atetea viongozi ‘waasi’ wa ODM

Na CECIL ODONGO, KEVIN CHERUIYOT January 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

BINTIYE marehemu Raila Odinga, Winnie, Jumapili, Januari 18, 2026 alionekana kutofautiana na amu yake, Dkt Oburu Oginga, akiapa kuwa hakuna atakayefurushwa ODM na kukosoa jinsi chama kinavyoendeshwa.

Bi Winnie, jana alijitambulisha na mrengo unaopinga uongozi wa Dkt Oginga ndani ya ODM ambao umekuwa ukishinikiza kuandaliwa kwa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) ili viongozi wateuliwe rasmi.

Mrengo huo wa viongozi waasi wa ODM ambao pia ni mwiba kwa Serikali Jumuishi, unashirikisha Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna na Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi.

“Wanaongea sana na tukiuliza maswali wanasema tutoke kwenye chama. Tukitaka watabaki na nani kwenye hiki chama? Hiki chama ni cha wananchi. Tukitoka wananchi nao wanaenda! Leo naleta salamu kutoka kwa ndugu zangu Babu Owino na Katibu Mkuu wa chama Edwin Sifuna,” akasema Bi Winnie akizungumza katika mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Kamukunji, eneobunge la Kibra, Nairobi.

“Baada ya baba kuaga dunia, abiria walichukua usukani na kuanza kutusukuma kila mahali ndani ya gari kama magunia,” akasema.

Bi Winnie ambaye ni mbunge katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), aliahidi kwamba atakuja na Bw Sifuna na Babu kwenye mkutano wa kisiasa atakaoandaa eneo hilo siku zijazo.

Bintiye Raila aliyeonekana kumezea ubunge wa Kibra katika uchaguzi mkuu ujao hasa baada ya kuahidi kusuluhisha tatizo la maji na umeme katika eneo hilo, alisema kuwa baadhi ya viongozi wa ODM wanajaribu kumuiga Raila ilhali hawawezi kutoshea kwenye viatu vyake.

“Baba hakuwa kibaraka na wale wanaodai aliwaambia hili au lile, wanamkosea heshima. Hakuwahi kusema ODM iko upande huu au ule,” akasema akionekana kupinga maoni ya baadhi ya viongozi wa ODM kuwa Raila aliwaambia wabakie katika Serikali Jumuishi.

Bi Winnie alisema sasa anategemea NDC kulainisha na kuzima wapinzani ambao wameteka ODM.

“NDC itakuwa moto, tutakutana nao huko,” akasema.

Hata hivyo, mkutano huo wa Bi Winnie haukuhudhuriwa na wabunge wa ODM isipokuwa madiwani kadhaa kutoka Kaunti ya Nairobi waliohudhuria na kuomba atengewe nafasi ya uongozi ODM.

Hii si mara ya kwanza ambapo mbunge huyo anatoa wito wa kuandaliwa kwa NDC. Katika Kongamano la Kuadhimisha Miaka 20 ya ODM jijini Mombasa mnamo Novemba mwaka jana, Bi Winnie alipendekeza chama kiandae NDC ili kupata wawakilishi wake katika ushirikiano na UDA ndani ya Serikali Jumuishi.

Hata hivyo, pendekezo hilo lilipingwa na Dkt Oginga aliyesema kuwa hawezi kumsaliti nduguye (Raila) na kwamba alikuwa akishirikishwa katika masuala yote yanayohusu ushirikiano huo, Raila alipokuwa hai.

Mnamo Januari 14 wiki jana, akihutubia umma katika eneobunge lilo hilo la Kibra, Dkt Oginga alisema hawatafukuza yeyote ndani ya ODM ila wanaotaka kuondoka wana hiari ya kujiondoa badala ya kukisambaratisha chama ndani kwa ndani.

“Kama ODM lazima tujiandae na hilo litafanyika tu ikiwa tuko pamoja. Hatuna nia ya kumfukuza mtu yeyote ODM, iwapo wanataka kuondoka wafanye hivyo kwa hiari,” akasema Dkt Oginga.

Uhasama kati ya Dkt Oginga na Bi Winne unaendelea kutokota zaidi huku mbunge huyo wa EALA akisusia vikao vya ‘Linda Ground’ ambavyo vimekuwa vikiendelea Magharibi mwa nchi.

Vikao hivyo vilifanyika wikendi katika kaunti za Busia na Kakamega, vikilenga kudhibiti umaarufu wa chama miongoni mwa jamii ya Mulembe.

Dkt Oginga, magavana Ferndandes Baraza (Kakamega), Dkt Paul Otuoma (Busia), Simba Arati (Kisii), Mwenyekiti Gladys Wanga na wajumbe wa chama mashinani walihudhuria mikutano hiyo.

Akiwa Kakamega, Dkt Oginga alikumbana wazi na uhasama wa kisiasa kati ya Gavana Barasa na Mbunge wa Lugari Nabii Nabwera ambao waliandaa mikutano tofauti ya wajumbe wa ODM.

Wawili hao wamekuwa wakizozania uenyekiti wa chama katika kaunti hiyo.

Seneta huyo wa Siaya alihudhuria mkutano wa Bw Nabii katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Emabole, Butere kisha akasafiri kwa helikopta hadi Hoteli ya Golf kuwahutubia wajumbe wa ODM wanaoegemea mrengo wa Bw Barasa.

“Nimeona mahali ambapo shida ipo na nitafanya kazi pamoja na Waziri Wycliffe Oparanya kuzitatu ili chama kiungane na kuwa imara,” akasema Dkt Oginga.

Bw Sifuna na Naibu Kiongozi wa chama hicho Geodfrey Osotsi walisusia mikutano ya ODM ilhali wanatoka ukanda wa magharibi mwa nchi.