Ruto achukua washauri wa kiuchumi wa Raila
RAIS William Ruto amewachukua baadhi ya wapangaji mikakati waliokuwa wakihudumu katika ODM chini ya aliyekuwa waziri mkuu marehemu Raila Odinga kumsaidia katika safari ya kuhakikisha nchi inapiga hatua kimaendeleo na kiuchumi.
Hii inafasiriwa kama mbinu ya hivi punde ya Rais kuwavutia viongozi wa ODM na kutwaa ngome ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Taifa Leo imebaini kuwa Rais Ruto ameamrisha wakuu wake wa kitengo cha kiuchumi wakiongozwa na Dkt David Ndii washirikiane na wataalamu wa kiuchumi waliokuwa katika kambi ya Bw Odinga.
Wapangaji mikakati hao ni Prof Anyang’ Nyong’o, Prof Karuti Kanyinga, Prof Michael Chege na Prof Oduor Wanyande.
Kazi ya washauri hao wa kichumi ni kuibuka na sera ya kupaliza Kenya hadi ifikie kiwango cha mataifa yaliyoendelea kiuchumi duniani kama Singapore.
Prof Kanyinga na Wanyande walikuwa na jukumu muhimu katika kutengeneza manifesto ya Azimio la Umoja hasa kitengo cha kiuchumi katika uchaguzi wa 2022 ambao Raila alipeperusha bendera ya muungano huo.
Wengine wanaojiunga na wataalamu hao ni Dennis Onyang ambaye alikuwa Msemaji wa Bw Odinga, na pia George Omondi.
Kujumuishwa kwa wanamikakati hao kunaongeza idadi ya wandani wa Bw Odinga ambao wamejiunga na kambi ya Rais Ruto ndani ya Serikali Jumuishi ambayo ilibuniwa baada ya maandamano ya Gen-Z mnamo 2024.
Prof Makau Mutua, mwandani wa Bw Odinga aliteuliwa mnamo Aprili 2025 kama Mshauri Mkuu kuhusu Masuala ya Katiba katika Afisi ya Rais.
Prof Adams Oloo, Joe Ager na Dkt Silvestor Okumu Kasuku ambao pia ni wandani wa Bw Odinga pia wamejiunga na kambi ya Rais kama washauri kiuchumi.
Ijumaa iliyopita, Prof Nyong’o aliongoza kikosi kilichowasilisha stakabadhi ya mageuzi ya kiuchumi kwa Rais Ruto katika ikulu ya Nairobi.
Stakabadhi ina mada ‘Maendeleo na Ruwaza Mpya ya Kiuchumi ya Kukweza Kenya hadi Nchi iliyopiga Hatua Kiuchumi’.
Rais alimsifu Prof Nyong’o kwa mchango wake kupitia stakabadhi hiyo aliyosema inaoana na Ruwaza ya 2030.
“Sote tutashirikiana kuhakikisha mipango ya maendeleo ya kiuchumi ya taifa hili inatekelezwa kuhakikisha Kenya inapiga hatua na kufika kiwango cha Singapore,” akasema Rais Ruto.