Mwanahabari wa Ivory Coast akosoa Kenya, Uganda na TZ kuandaa AFCON 2027
MWANAHABARI mkongwe wa michezo raia wa Ivory Coast Mamadou Gaye, ameshambuliwa vikali na wadau wa soka nchini, baada ya kusema kwamba, inakuaje Kenya Uganda na Tanzania wanandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 bila barabara.
Mataifa hayo matatu yamepangwa kuwa wenyeji michuano hiyo kuanzia Juni 19 hadi Julai 18.
Gaye ambaye ni mchambuzi wa Soka ya Afrika na mshauri wa Soka ya Afrika Magharibi, aliuliza swali hilo wakati wa kikao cha waandishi wa habari na rais wa Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe nchini Morocco Jumamosi, kuelekea fainali ya jana ya AFCON kati ya wenyeji Morocco na Nigeria.
“AFCON inayofuata itaandaliwa Afrika Mashariki ambako tayari nimekwenda. Hakuna barabara ndani ya nchi, wenzangu waliniambia kutoka nchi moja hadi nyingine, itakuchukua siku mbili kuendesha gari. Hili haliwezi kushusha hadhi ya AFCON? Kuna uwezenako michuano hii ikaandaliwa katika taifa lingine?” Gaye aliuliza.
Katika kumjibu, Motsepe alisema: “Nina wajibu wa kuendeleza soka kote Afrika. Siwezi kuwa na mashindano hayo katika nchi hizo nne tu ambazo zina miundombinu. Lazima utengeneze fursa kwa nchi zingine kujenga miundombinu katika kiwango cha kuandaa Kombe la Dunia na kuendeleza soka katika nchi hizo pia. Nina imani kwamba AFCON nchini Tanzania, Kenya na Uganda itafanikiwa sana.”
Aidha aliongezea akisema, “Hata Kombe la Dunia la mwaka huu nchini Marekani, Canada na Mexico kutakuwa na changamoto. Ndio maana nilihakikisha kwamba, mataifa hayo matatu yanaandaa CHAN 2024 hata ingawa mataifa hayo kuwa tayari kwa mandalizi ya AFCON.”
Wakenya mitandaoni walikerwa na Gaye kupitia video hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
“Ulikuwa Kenya wakati wa CHAN, ilikuchukua siku ngapi kutoka Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo au Kasarani hadi hoteli ya Kempinski au JW Marriott? dakika tu, sio siku. Uliona na ulipata kwa urahisi, sio machafuko unayoyazungumzia katika video hiyo,” alisema Ustadh Okello Kimathi katika chapisho ndefu kwenye mtandao Facebook.
“Swali la ajabu sana. Natumai kumuona nchini 2027,” aliandika Mkuu wa Mawasiliano, Vyombo vya Habari na Uhusiano wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Jeff Kinyanjui kwenye ukurasa wa X.
“Hebu fikiria raia wa Ivory Coast akiongea vibaya kuhusu Afrika Mashariki? Ivory ya nchi zote?” Asher Omondi alisema kwenye jukwaa hilo hilo.
Frère Jules Weston alichapisha kwenye jukwaa hilo hilo: “Nchi yake yenyewe bado inatatizika na utawala inalinganishwa na Kenya? Watu wake wenyewe wanacheza soka ya kulipwa huko Tanzania, wengine wako Kenya wakifanya kazi za kila aina ili kujikimu kimaisha.”
Hata hivyo, baadhi ya watu mtandaoni wamemtetea Mamadou.
“Kile ambacho huyu jamaa anasema ni kweli 100% kuhusu hali ya mawasiliano kwa barabara kutoka eneo la viwanja vinavyoandaa mashindano katika nchi moja ya Afrika Mashariki hadi nyingine,” aliandika George Omwomo kwenye X.
“Ni wazi tuna barabara, lakini kuna hoja ya kuzingatiwa hapa. Hata tukisema tutakuwa tayari ifikapo 2027. Angalia usafiri wa umma, usalama, huduma za dharura, na kadhalika,” alisema Plotwise kwenye X.