Akili MaliMakala

Anavyounda mamilioni kupitia biashara ya moringa

January 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

ALIPOPATA kifungua mimba wake, Elizabeth Mwenda hakutarajia kushuhudia upungufu wa maziwa – ya mama anayenyonyesha.

Alikosa kabisa maziwa, jambo analohoji lilisumbua sana malaika wake ikizingatiwa kuwa ni ‘chakula kinywaji’ muhimu sana kwa mtoto anapozaliwa.

“Nilijifungua lakini sikuwa na maziwa ya kutosha mtoto kunyonya. Mama mkwe wangu alidhani sikuwa nakula vizuri, lakini hata baada ya kujaribu kila ushauri, hakuna kilichobadilika,” anakumbuka.

Mume wake, aliyekuwa akifanya kazi na wakulima kupitia shirika lisilo la kiserikali, alitafuta msaada kutoka kwa jamii alizokuwa akihudumia.

Majibu, Elizabeth anasema yalikuwa rahisi lakini ya kushangaza: moringa.

Elizabeth Mwenda akielezea kuhusu kilimo na uchakataji wa moringa. Picha|Sammy Waweru

Mume wake, anasimulia kwamba alirudi nyumbani na mfuko mdogo wa majani ya moringa, mmea ambao mwaka 2007 haukujulikana sana nchini Kenya.

“Niliamua kuujaribu licha ya kutokuwa na uhakika,” Elizabeth anasema.

Ndani ya saa chache baada ya kutumia kijiko kimoja cha unga wa moringa kwenye uji, mwili wake ulibadilika haraka.

Tatizo la upungufu wa maziwa lilitatuliwa kabisa. Nilianza kuzalisha maziwa kwa wingi kiasi kwamba nilikuwa nikikama upande mmoja huku mtoto akinyonya upande mwingine, anasimulia mama huyo.

Alichoshuhudia kilimpa imani kubwa kuhusu tija kiafya za moringa. Hapo ndipo safari ya Botanic Treasures ilipoanza.

Green Gold, mojawapo ya bidhaa zinazoundwa na Elizabeth Mwenda kwa kutumia moringa. Picha|Sammy Waweru

Akiwa na hamu ya kuelewa zaidi, Elizabeth alianza kufanya utafiti kuhusu moringa na kugundua kuwa ingawa mmea huo ulikuwa umefanyiwa tafiti nyingi kimataifa, Wakenya wachache hawakuufahamu.

Mwaka 2008, yeye na mume wake walianza biashara ya moringa kwa mtaji wa Sh5, 000, wakinunua kilo saba za majani makavu kutoka kwa wakulima.

Aidha, walikuwa wakiisaga, kupakia na kuhamasisha kisoko kwenye maonyesho ya kilimo kama yale ya kibiashara na kilimo Nairobi, ASK.

“Tulizamia kuhamasisha wananchi kuhusu faida kiafya za moringa,” Elizabeth akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee.

Hata ingawa wengi hawakuwa wakiamini bidhaa za mitishamba, wanandoa hao waliendelea bila kukata tamaa.

Elizabeth Mwenda akionyesha mojawapo ya bidhaa aliyochakata kwa kutumia mtishamba aina ya moringa. Picha|Sammy Waweru

Baada ya miaka minne ya kufanya kazi na wakulima na kuwatafutia masoko yenye ushindani mkuu, walisajili rasmi Botanic Treasures mwaka wa 2012.

Leo hii, kampuni hiyo huchakata hadi kilo 2,000 za moringa kila mwezi na hushirikiana na zaidi ya wakulima 300 kote nchini.

Bidhaa zake ni pamoja na unga, chai, mafuta, na vinywaji vyenye ufaafu kiafya vilivyowekwa kwa muda kuchacha.

Manufaa ya moringa kiafya

Moringa, ikijulikana kama ‘mti wa miujiza’ imesheheni virutubisho, kuanzia Vitamini A, C, E na B, na madini; ironcalciumpotassiummagnesium, na zinc.

Manufaa mengine ya mtishamba huo ni kushamiri protein, na fiber, ukisifiwa kukabiliana na changamoto za tumbo hasa wanaougua vidonda vya tumbo na asidi.

Elizabeth Mwenda akipanga bidhaa za moringa kwenye maonyesho Westlands, Nairobi. Picha|Sammy Waweru

Hali kadhalika, moringa inatajwa kusaidia chakula kusagika tumboni upesi, kushusha athari za maradhi ya Kisukari, na pia kulainisha ngozi na nywele.

Mmea huu ni kati ya inayonawiri maeneo kame (ASAL). Mbali na Meru na Tharaka Nithi, kaunti zingine zizozalisha moringa ni Makueni, Kilifi, Machakos na Marsabit.

Hata hivyo, sehemu zinazopokea mvua wapo wakulima wanaoukuza.

Licha ya tija hizo, sekta ya mitishamba, hata hivyo, haikosi changamoto kisoko. Elizabeth, anataja hatua ndefu kusaka leseni hasa ya kuuza bidhaa nje ya nchi kama kibarua kwa wafanyabiashara washirika na wakulima.

Bidhaa ya kusaidia tumbo – probiotic iliyoundwa kwa kuchakata moringa. Picha|Sammy Waweru

Kwa sasa, Botanic Treasures inashughulikia vibali vya kuuza bidhaa zake Germany na Sweden.

Biashara ilipoanza, wafanyakazi walikuwa Elizabeth, mume wake na watoto wao wadogo, na sasa kampuni hiyo imestawi kiasi kuwa imeajiri wafanyakazi 16 wa kudumu na vibarua wapatao 60 – haswa misimu ya upanzi.

Kutoka kwa ekari nne walizoanza nazo kulima moringa, sasa wanamiliki zaidi ya 15.

Botanic Treasures ilikuwa miongoni mwa waonyeshaji walioshiriki Warsha ya Bioeconomy Cluster Development Workshop, iliyoandaliwa mnamo Novemba 6 na Stockholm Environment Institute (SEI) Jijini Nairobi, mwaka uliopita, 2025.

Hafla hiyo ilileta pamoja wafanyabiashara kutoka sekta mbalimbali kujadili mikakati kuboresha biashara.

Elizabeth Mwenda aliingilia biashara ya moringa alipopata ujauzito wa kifungua mimba wake. Anakiri ni biashara yenye hela. Picha|Sammy Waweru