Habari za Kitaifa

Mvulana aliyeitwa shule ya Alliance anaokota chupa kutafuta karo

Na STEVE OTIENO January 20th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MWANAFUNZI aliyeibuka miongoni mwa waliopata matokeo bora zaidi katika kundi la kwanza lililofanya Mtihani wa Gredi ya 9 (KJSEA)amegeukia kuchakura biwi la taka akijaribu kusaka hela za karo.

John Mwalili, 15, aliyekuwa akisomea shule ya msingi ya Zau, Athi River, Machakos, alizoa alama 64 na kuwaacha kwa mbali wenzake kwani mwanafunzi aliyemfuata alizoa alama 54.

Alama zake zilimshindia nafasi katika mojawapo ya shule za upili za kifahari zaidi nchini, Alliance.

Miezi michache kabla ya kufanya mtihani, John, anayeishi na familia yake mtaani Kware, alidiriki kulenga juu. Alipokuwa anajaza shule za kitaifa (C1), alichagua Shule ya Upili ya Alliance kwanza kisha Nairobi School na Upperhill.

Siku ya shule, John angeondoka nyumbani saa kumi alfajiri kusafiri hadi Athi River na kurejea saa tatu usiku.
“Nilijua elimu ndiyo fursa yangu pekee,” alisema.

Wanafunzi walioitwa Alliance waliripoti Januari 12.

Zaidi ya wiki moja baadaye, John amesalia nyumbani kwao Kware, akiwatazama wenzake wakienda shuleni na kuendeleza masomo yao.

Ujumbe wa matokeo na shule aliyoitwa ulipowasili, familia ilisherehekea kwa muda kabla ya uhalisia kujitokeza.

John alipogundua wazazi wake hawangemudu karo na mahitaji ya shule, alifanya uamuzi mchungu na kuanza kuchakura biwi la taka la Kware kujaribu kukusanya hela za kumwelimisha.

Taifa Leo ilipomtembelea Kware, Nairobi, John alikuwa bado ameikunja vyema barua yake ya kuitwa shule na kuihifadhi katika kijisanduku cha chuma, kana kwamba alihofia kuishikashika kungesababisha ndoto yake kutoweka.

Kilo moja ya chupa za plastiki zinazookotwa huuzwa Sh3 tu.John amefanikiwa kukusanya karibu kilo 100, na kupata Sh300, kiasi kinachoashiria pengo kati ya juhudi zake na gharama ya kujiunga na shule.

Shule ya Upili Alliance inatoza karo ya Sh53,500 kwa mwaka lakini kiasi hicho ni sehemu tu ya mzigo.

Ukijumuisha sare za lazima, malazi, vyombo vya kulia, vifaa vya kibinafsi, vifaa vya masomo na mavazi ya ziada, kwa jumla, kulingana na baba yake Nicholas Mwalili, gharama ya kujiunga na shule hiyo ni takribani Sh120,000.

“Siyo karo tu. Ukiongeza kila kitu kinachohitajika, linakuwa jambo It is not just the fees. When you add everything required, it becomes impossible for me to raise on my own,” Mr Mwalili.

Kufikia sasa, baba huyo amemudu tu kununua kijisanduku cha chuma, kifaa kipya wanachobeba wanafunzi kwenda shule za bweni.

Sare bado haijanunuliwa na inaweza kutolewa tu John atakapojiunga rasmi na shule.

Familia hiyo imeomba usaidizi kutoka kwa viongozi eneo hilo, akiwemo diwani wa Kware na Gavana, lakini juhudi zao zimegonga mwamba.