Maoni

Wabunge watajificha wapi baada ya Ndindi Nyoro kupunguza karo Kiharu?

Na HELLEN NJAGI January 20th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro amewavua nguo wenzake kwa kutekeleza sera za elimu badala ya kupiga domo tu kwenye eneobunge lake.

Kulingana naye, elimu inafaa kupewa mgao zaidi wa fedha katika bajeti ya kila mwaka nchini.

Katika eneobunge analoongoza la Kiharu, mbunge huyo ameipunguza ada ya sekondari ya kutwa kutoka Sh1,000 kwa mwanafunzi kila muhula hadi Sh500.

Bw Nyoro ametekeleza haya kupitia mpango unaojulikana kama ‘Masomo Bora’.

Zaidi ya hayo, mpango huo umewapa wanafunzi katika shule za sekondari za kutwa chakula cha mchana na vifaa vya kujifunzia huku wabunge wengine wakiwa kwenye misafara ya vyama wakitafuta nafasi ya kuchaguliwa kwa muhula mwingine.

Bw Nyoro amezidisha motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vyema katika ufunzaji na ujifunzaji katika eneo hilo.

Isitoshe, kupitia kwa mitandao ya kijamii, ameonyesha nchi nzima jinsi alivyojitahidi kujenga shule mpya na kukarabati miundomsingi katika shule ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Haya yameonekana mageni kwa wabunge wenzake.

Wiki jana alipotangazia wakazi wa Kiharu kuwa atapunguza karo, aliibua maoni mbalimbali kwa wananchi na viongozi wa kisiasa nchini.

Baadhi yao wamemsifu kwa mpango wake wa ‘Masomo Bora’.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wabunge ambao wamemkashifu Bw Nyoro kwa kusema kuwa eneobunge lake lina walimu wa kutosha kwa hiyo hatumii mgao wake wa fedha za maendeleo ya eneobunge kuwalipa walimu kama wanavyofanya wabunge wengine.

Je, kwa nini eneobunge hilo likawa na walimu wa kutosha huku shule katika baadhi ya maeneobunge nchini zikiwa na asilimia themanini ya walimu kama walivyodai baadhi ya wabunge?

Huku ni kusema kuwa wabunge wanaowawakilisha wananchi wamezembea kimaksudi na kukosa kuhakikisha kuna usawa katika sekta ya elimu nchini Kenya ingawa ukweli wanaujua.

Pia, wapo viongozi wa kisiasa waliomkashifu Bw Nyoro kwa kudai kuwa alikuwa mwenyekiti wa kamati ya bajeti bungeni kwa hivyo alitumia nafasi hiyo kunufaisha eneo lake.

Haya ni madai ya kuajabisha kwani ni jambo lililo wazi kuwa kamati ya fedha ndiyo iliyo na jukumu la kutoa mgao wa fedha za serikali.

Wengine wamedai kuwa hawajatekeleza miradi mingi kama alivyofanya Bw Nyoro kwa sababu inalingana na jinsi mtu alivyojipanga.

Ikiwa kutekeleza miradi inalingana na jinsi kiongozi alivyojipanga basi, pongezi inawaendea wapigakura wa Kiharu kwa kuchagua akili badala ya ubahili.

Kwa baadhi ya viongozi, Bw Nyoro amewapalia makaa kichwani kwani wananchi wanapolinganisha maendeleo ya eneobunge lake na maeneobunge mengine, wabungewenza wanabaki wakichutama ndimi zao zikikwama kooni.

Hongera Bw Nyoro kwa kuwazindua wananchi na kuwaacha na taswira kuwa maendeleo katika maeneobunge yanawezekana.

Heko tena kwa kukwepa tabia ya kujiunga na misafara ya baadhi ya wanasiasa kuziimba pambio za ‘wantam’na ‘tutam.’

Badala ya kukashifu hatua alizopiga, kila mbunge akadirie aliyotekeleza.

Eneobunge la Kiharu liwe kielelezo hata kwa wananchi wenye hulka ya kutaka wanaogombea viti vya kisiasa kuwapa hela ili wawachague.

Pia ni funzo kuwa baada ya uchaguzi wananchi wasiwafuate viongozi kwa kutaka kupewa zawadi ndogondogo bali waitishe miradi itakayodumu na kuinua uchumi wa jamii nzima.