Habari za Kaunti

Mbunge sasa ajitetea kuwa asilinganishwe na Ndindi Nyoro wa Kiharu

Na WINNIE ATIENO January 20th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Kinango, Bw Gonzi Rai, ametetea viongozi wa eneo la Pwani wanaolaumiwa na wananchi kwamba wameshindwa kuwekeza katika elimu.

Wakazi walianza kufananisha uwekezaji wa viongozi wa Pwani katika sekta ya elimu na yale wanayoona yakitendwa katika eneobunge la Kiharu, Kaunti ya Murang’a. Mbunge wa eneo hilo ni Bw Ndindi Nyoro.

Kulingana naye, Murang’a kuna utajiri kwa sababu wanategemea kilimo. Alisema sehemu za Pwani hazifai kufananishwa na kwingine kwa sababu kuna athari za ukame na watu wengi hutegemea misaada.

“Katika shule nyingi za sehemu hiyo wanafunzi wengi ni watoto wa wakulima na zina idadi ndogo,” alidai Bw Rai.

Alieleza kuwa, alipoanza kazi kama mbunge alipata shule sita pekee katika eneobunge lake lakini sasa zimefika 36.

“Kuna nyingine sita nataka kujenga. Nataka kuwaambia wanachi yale yanayofanywa na Bw Nyoro ni kwa sababu kule aliko ni tofauti. Vilevile mazingira yetu ni tofauti, huku kwetu mtoto anaweza kufika Gredi ya 9 na akakomea hapo kwa sababu mzazi hana fedha za kuendeleza,” alisema Bw Rai.

Hata hivyo, alisema kwa sasa viongozi wa Pwani wameungana na hawatakubali tena ubaguzi kwenye ugavi wa miradi ya maendeleo na bajeti.