Hatua ya Wizara ya Elimu kukumbatia teknolojia ni ya kupongezwa
HATUA ya Wizara ya Elimu, kupitia Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC), ya kuruhusu watahiniwa wa KCSE 2025 kuangalia matokeo yao kupitia tovuti badala ya kutumia huduma ya SMS ni uamuzi unaostahili kupongezwa.
Huu ni ushahidi tosha kuwa sekta ya elimu nchini inaelekea katika mwelekeo sahihi wa kidijitali.
Kwa miaka mingi, mfumo wa SMS umekuwa ukikumbwa na changamoto tele, zikiwemo ucheleweshaji wa ujumbe, gharama za huduma, hitilafu na hata visa vya ulaghai.
Watahiniwa na wazazi wengi wamewahi kupitia hali ya sintofahamu wakisubiri ujumbe ambao wakati mwingine unakosa kurudi.
Mfumo wa mtandaoni, kwa upande mwingine, unatoa uwazi, ufanisi na usahihi zaidi.
Kupitia tovuti ya KNEC, mtahiniwa anapata matokeo yake moja kwa moja bila kupitia wahusika wa kati.
Hili linaongeza imani ya umma katika mfumo wa mitihani ya kitaifa na kuondoa hofu ya upotoshaji wa matokeo.
Aidha, mfumo huu unawezesha uhakiki wa haraka kwa kutumia nambari ya mtihani na jina lililosajiliwa, hatua inayoongeza usalama wa taarifa za watahiniwa.
Uamuzi huu pia unaendana na juhudi za serikali katika kuendeleza ajenda ya mageuzi ya kidijitali nchini.
Kadiri Kenya inavyozidi kukumbatia teknolojia katika utoaji wa huduma za umma, ndivyo huduma zinavyokuwa nafuu, za haraka na zinazowafikia wananchi wengi zaidi.
Ni kweli kwamba si kila Mkenya ana ufikiaji wa mtandao wa intaneti, lakini hatua hii inaweka msingi mzuri, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya kidijitali shuleni na maeneo ya mashinani.
Kwa jumla, Wizara ya Elimu imeonyesha uongozi thabiti na wa kisasa.