Okanga aachiliwa kesi dhidi ya Ruto aliyopambana mwaka mmoja na nusu
MFUASI sugu wa aliyekuwa kinara wa ODM Raila Odinga aliyeshtakiwa kwa kuchochea ghasia kwa madai ya kutaka Rais William Ruto apigwe risasi ameachiliwa huru na mahakama ya Milimani.
Nuru Okanga aliachiliwa na mahakama ya Milimani ambapo alipambana na kesi hiyo kwa mwaka mmoja unusu.
Okanga aliyetetewa na mawakili 10 aliondoka kizimbani kwa furaha huku akiahidi “kuendelea na mapambano ya kuhakikisha wanyonge nchini wamepata haki na wanasiasa majitu hawawanyanyasi wananchi.”
Mbali na kuendeleza shinikizo za haki kwa kila mmoja, Okanga alisema pia “atatumia muda mwingi kusoma kwa vile yuko shule ya sekondari.”
“Nitatumia muda mwingi sasa kusoma nijiboreshe kimasomo na nipite mtihani wa KCSE,” alisema Okanga.
Alisema kwamba alikuwa nyumbani tangu Raila afariki na alirudi Januari 18, 2026 kuhudhuria kesi hii ambayo imening’inia shingoni mwake kwa muda wa mwaka mmoja unusu.
“Naishukuru mahakama kwa kuzingatia haki na sheria. Namshukuru hakimu kwa kutathmini kwa kina ushahidi wote na kufikia uamuzi sikufanya makosa yoyote na wala sikuvunja sheria,” Okanga alimweleza hakimu na wanahabari waliofurika mahakama ya Milimani.

Ikimwachilia huru Okanga, Mahakama ilisema upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha madai kwamba mwanaharakati huyu wa kisiasa alichapisha katika mitandao ya kijamii habari za uchochezi.
Okanga alikabiliwa na mashtaka ya kumtaka aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua atumie mafunzo yake ya Afisa tawala na kujihami kwa bastola na kumchapa risasi Rais Ruto.
Hakimu alisema baada ya kuchambua ushahidi wote uliowasilishwa kortini alifikia uamuzi kwamba “polisi walishindwa kuthibitisha habari zilizochapishwa katika mitandao mbali mbali ziltumwa na Okanga.”
Hakimu mwandamizi Rose Ndombi alisema polisi walikiri mbele yake kwamba hawakuwa na ujuzi wa kubaini na kung’amua habari zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii zilitoka kwa simu ya Okanga.
Bi Ndombi alisema baadhi ya mashahidi waliofika kortini waliungama kwamba ushahidi waliowasilisha ulitoka kwa mamlaka ya mawasiliano nchini CAK na ilikuwa ngumu kuthibitisha ufaafu wake.
Hakimu alisema baadhi ya mashahidi ambao walikuwa polisi walitapatapa huku na kule na kushindwa kabisa kuthibitisha kesi dhidi ya Okanga.
Mahakama ilisema ushahidi kamili haukuwasilishwa kortini kumhusisha kabisa Okanga na video zilizokuwa zikitamba mitandaoni.
Mbali na kumwachilia Okanga, hakimu alikashfu polisi kwa kumkamata na kumfungulia mashtaka wakijua kabisa hakuhusika na video zilizozagaa mitandao ya kijamii.
Mawakili 10 waliomtetea Okanga wakiongozwa na Babu Owino na Shadrack Wambui walisema wataishtaki Idara ya Polisi kwa kumfungulia mashtaka ya uwongo.
“Tutaomba mahakama kuu iamuru Okanga alipwe fidia kwa kuteswa na polisi walipomzuilia siku 21 bila sababu. Kesi hii itakuwa funzo kwa idara ya polisi kwamba wasikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa,” Wambui alimweleza hakimu.