Habari za Kaunti

Hofu ukabila sasa ukiteka siasa za ugavana Mombasa

Na MWANDISHI WETU January 21st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI katika Kaunti ya Mombasa wamehimiza wanasiasa na raia kuepuka siasa za ukabila.

Kwa miezi kadhaa sasa, kaunti hiyo imeshuhudia kampeni za mapema za ugavana ambapo baadhi ya wale wanaolenga kuwania wadhifa huo wamelaumiwa kwa kutoa matamshi yanayoweza kugawanya wananchi kwa mirengo ya kikabila.

Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, alionya kuwa, siasa za ukabila zimepitwa na wakati na zitarudisha nyuma hatua zilizopigwa kufikia sasa kimaendeleo.

Katika mkutano na wawakilishi wa jamii kutoka Wadi ya Shanzu afisini mwake Jumatatu, Bw Nassir alieleza kuwa, wanasiasa wanafaa kushindana kwa misingi ya ruwaza na uwezo wa kuhudumia wananchi badala ya migawanyiko.

“Mombasa lazima ikatae kabisa wachochezi wa ukabila ambao hawaezi kushindana kwa maono, kwa hivyo wanataka kujisitiri kwa migawanyiko. Tumepiga hatua kubwa sana na tumefanya bidii mno kujenga umoja na uwiano wa kijamii kiasi cha kwamba hatuwezi kuruhusu mtu yeyote aturudishe nyuma hadi kwa siasa za kidini, kikabila wala rangi,” akasema.

Alisema mikutano anayoandaa na wananchi wa wadi tofauti za kaunti imekusudiwa kusikiliza masuala ambayo jamii zingependa kupewa kipaumbele, kuelewa changamoto zinazowakumba, na kukubaliana kuhusu hatua ya pamoja ya kuzisuluhisha.

Kufikia sasa, wanasiasa ambao wameonyesha nia ya kutaka kumng’atua Bw Nassir katika uchaguzi wa mwaka ujao ni Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, aliyekuwa Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, Katibu Mkuu wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Hassan Omar, na Spika wa Bunge la Kaunti ya Mombasa, Bw Aharub Khatri.

Suala la migawanyiko kwa misingi ya kikabila au dini katika Kaunti ya Mombasa ni zito, ikizingatiwa kuwa, eneo hilo limewahi kushuhudia mauaji yaliyochochewa kwa misingi hiyo.

Baadhi ya matukio ya kutisha yaliyosababishwa na uchochezi aina hiyo katika miaka iliyopita ni kama vile mashambulio ya Kaya Bombo dhidi ya jamii zilizodaiwa si wenyeji wa Mombasa, na mashambulio ya kigaidi yaliyochochewa kidini.

Akiongea hivi majuzi katika eneobunge la Likoni, Bw Khatri alikosoa wanaoendeleza siasa za chuki akisema watu washindane kwa misingi ya maendeleo.

“Haya ndio maendeleo tunayotaka, hatutaki siasa za chuki. Hatutaki siasa za ukabila. Siasa nzuri tutaleta ni maendeleo,” akasema, katika mahafali ya mpango wa kuwawezesha vijana.

Msimamo sawa na huu ulitolewa awali na Bw Mbogo, ambaye ndiye mwenyekiti wa bodi ya mradi wa Uchukuzi wa Bandari ya Lamu-Sudan Kusini-Ethiopia (LAPSSET).

Bw Mbogo alisema makabila mengi yameishi Pwani kwa amani kwa miaka mingi na hata kuoana kwa hivyo hakuna atakayeruhusiwa kuanzisha siasa za ukabila kuelekea 2027.

“Hatutakubali kiongozi ambaye anakuja hapa kutuletea siasa za kikabila,” akasema.

Bw Ali, maarufu kama ‘Jicho Pevu’, alijitenga na madai kwamba ndiye anaeneza siasa za ukabila.

Kupitia mitandao ya kijamii, mbunge huyo anayeegemea upande wa aliyekuwa naibu rais, Bw Rigathi Gachagua, alisema wanaodai anatafuta kura kupitia ukabila wamegundua ana nafasi bora kushinda katika uchaguzi ujao wa ugavana.

“Huwezi kupumbaza raia ambao wamezinduka. Wakati huu wakazi wa Mombasa hawatapotoshwa kwa uongo na utapeli,” akasema.