Makala

‘Tulivyoua waumini 700 msituni’: Mkuu wa Ulinzi wa Pasta Mackenzie afunguka

Na BRIAN OCHARO January 21st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MMOJA wa wafuasi sugu wa Kiongozi wa Kanisa tatanishi la Good News International Ministries Paul Mackenzie, ametoa simulizi ya kutisha, akisema watu 700 walikufa wakifunga katika msitu wa Shakahola.

Mackenzie, anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya waumini 450 kutokana mafunzo ya itikadi potovu.

Akikamilisha kutoa ushahidi katika Mahakama Kuu ya Mombasa, Enos Amanya Ngala aliyekuwa mkuu wa ulinzi katika msitu wa Shakahola, Kilifi, alisema kuwa janga hilo halikusababishwa na uaminifu na hamu ya wokovu tu bali “ulaghai na woga uliogeuza utiifu wa kidini kuwa mtego”, kwa wafuasi wa dhehebu hilo.

Ngala, ambaye pia anajulikana kama,’Hallelujah’, alielezea jinsi yeye, na wafuasi wengine zaidi ya 1,000 wa Mackenzie, walitekeleza maagizo yake, hali inayoashiria kuwa hamna aliyetarajiwa kusalia hai katika msitu baada kufuata mafunzo hayo potovu.

“Ningependa kusema kuwa zaidi ya watu 700 waliaga dunia wakifunga Shakahola,” akasema.

Kinaya ni kwamba wakati ambapo wafuasi walikuwa wakifunga, Mkewe Mackenzie Rhoda Mumbua alikuwa akila vizuri na kuongeza hata matunda baada ya kushiba.

“Baada ya kutafakari kwa kina kuhusu shughuli zilizokuwa zikiendelea katika msitu wa Shakahola, nilijutia vitendo vyangu vilivyonifanya kupoteza pesa zangu kwa mhubiri tatanishi Paul Mackenzie na watoto wangu sita kutokana na mafunzo ya uwongo,” akasema mahakamani.

Ngala ni mshukiwa wa kwanza kukiri kosa katika kesi ya mauaji ya Shakahola yaliyofichuliwa 2022 na kuibua kero kubwa nchini na kimataifa.

Kulingana na maelezo yake, yaliyofanana na yale ya mashahidi wa awali, wafuasi wa dhehebu hilo waliwekeza pesa zao katika vipande vya ardhi walivyouziwa na mhubiri Mackenzie.

Lakini baadaye, walikabiliwa na tishio la kufurushwa kutoka kwa vipande hivyo vya ardhi walivyoamini kuwa walinunua kwa njia ya halali.

Kufikia Juni 2022, hofu na wasiwasi uliwakumba waumini hao katika msitu wa Shakahola, hali iliyofichua kuwa ahadi zilizowavutia katika msitu huo zilikuwa hadaa tupu.

Ni katika msingi huu wa wasiwasi na hisia za kusalitiwa ambapo waliamua kuanza kususia chakula kama “kinga dhidi ya shambulio la adui” ambaye waumini hao waliambiwa angewapata.

Ngala alihamia Shakahola mnamo Novemba 2020.

Kabla ya hapo, aliishi Nairobi na mkewe pamoja na watoto saba; na kulingana naye, hali yake kifedha ilikuwa thabiti. Pamoja na kakake mdogo, David Amanya, aliendesha biashara ya uzoaji takataka kwa jina Edmal Garbage Collection.

Walikodisha malori ya kusafirisha takataka hadi jaa la Dandora.

“Mapato niliyochuma kutoka kwa biashara hii yaliniwezesha kununua ploti na kujenga nyumba ya makazi katika eneo la Kasarani,” akasema.

Baada ya kujiunga na Kanisa la Good News International Ministries mnamo 2019, Ngala alijulishwa na Pasta George Mwaura, mshirika kwa karibu wa Mackenzie, kwamba mhubiri huyo alikuwa akiuza ardhi ya kilimo katika eneo la Shakahola.

Baada ya kuvutiwa na habari hizo, Ngala aliuza ardhi yake ya Nairobi kwa Sh700,000.

Alituma Sh100,000 kwa Mackenzie kama malipo ya awali ya kipande cha ardhi Shakahola na Sh100,000 zingine kwa mshirika wa mhubiri huyo.

Hii ni baada ya kushauriwa kwamba ni hatari kwake kusafiri na kiasi hicho cha pesa.

Alipowasili Malindi, Ngala aliomba kuonyeshwa kipande cha ardhi alicholipia Sh200,000.

“Mackenzie alinielekeza kwa Mwaura, niliyemuuliza kuhusu ardhi hiyo, lakini hakunijibu. Nilimwongezea Sh20,000 ili anionyeshe ardhi yangu lakini nilikaa kwa mwezi mmoja kabla ya kuonyeshwa ardhi hiyo,” akaeleza.

Hiyo ilikuwa mwaka wa 2021. Ngala alieleza mahakama kwamba baadaye Mwaura alimfichulia kuwa Mackenzie hakuwa akiuzia wafuasi wake ardhi, bali alikuwa akiwaruhusu kuishi katika shamba hilo kama maskwota.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani awali, pia ulionyesha jinsi waumini wengine walihangaishwa na kuhadaiwa kwamba wangeuziwa ardhi.

Baadaye Mwaura alimhamisha Ngala na waumini wengine hadi Ranchi ya Chakama, umbali wa kilomita tano kutoka Shakahola, ambako wafuasi wa Mackenzie walijenga makazi ya muda.