Habari za Kitaifa

Kioja OCS akibebwa hobelahobela na polisi wenzake kutoka mti aliokuwa akiukumbatia

Na VITALIS KIMUTAI January 21st, 2026 Kusoma ni dakika: 1

KULIKUWA na kioja Kaunti ya Kericho afisa wa ngazi ya juu kwenye idara ya polisi alipoamua kukumbatia mti, mtindo ambao sasa umechangamkiwa na Wakenya kama sehemu ya kudhihirisha maasi.

Afisa huyo alisema alichukua hatua hiyo kulalamikia dhuluma za kijinsia zinazowalenga wanawake na wasichana kote nchini.

Tukio hilo lisilo la kawaida lilifanyika katika kituo cha polisi cha Sosiot eneobunge la Belgut, Kericho.

Afisa Msimamizi wa Kituo (OCS) Kennedy Wanjala alipatikana amekumbatia mti akiwa amevalia sare ya kazi.

“Eneo lilitembelewa na ikathibitishwa OCS alikuwa akikumbatia mti akiwa amevalia sare. Hatua yake ilivutia wananchi wengi,” ikasema sehemu ya ripoti ya polisi.

Alipokuwa akikumbatia mti afisa huyo alisema “Niko hapa kulalamikia dhuluma za kimapenzi dhidi ya wanawake na wasichana kwa sababu unajisi na ubakaji umekuwa juu sana.”

Pia alilalamikia visa vilivyoongezeka vya matumizi ya dawa za kulevya.

“Matumizi ya dawa za kulevya yanawaathiri vijana na hili ni suala ambalo linastahili kushughulikiwa,” akaongeza.

Alipokuwa akikumbatia mti, wananchi nao waliendelea kumiminika hapo na kumtazama.

Bw Wanjala pia alitumia muda huo, saa nne na dakika 45 asubuhi ya Jumanne, Januari 20, 2026, kuwaonya wahalifu kuwa hawatawaachiliwa wakishanyakwa.

Hata hivyo, kioja kilishuhudiwa pale wenzake walipomtoa mtini na akapelekwa kufanyiwa uchunguzi wa kiakili.

Truphena Muthoni kutoka Kaunti ya Nyeri ndiye alianzisha zoezi la kukumbatia mti ambalo sasa limekuwa maarufu sana.

Alikumbatia mti kwa saa 72 mnamo Desemba 11 kuhamasisha umma kuhusu utunzaji wa mazingira.

Tangu wakati huo, Wakenya wengi wameiga tabia hiyo. Susan Njeri kutoka Nakuru ni wa hivi punde kufanya hivyo, alipokumbatia mti kuishinikiza serikali iangazie masaibu ya Wakenya wanaofanya kazi Saudi Arabia.

Hata hivyo, serikali imetoa onyo kuhusu tabia hiyo ikiihusisha na athari hasi kiafya.

Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni alionya kuwa kukumbatia mti kwa kipindi kirefu kuna athari zake.

Alitaja kisa cha James Irungu kutoka Murang’a ambaye alipata tatizo la figo baada ya kukumbatia mti kwa karibu saa 80.