Habari za Kitaifa

Wazee wa ukoo wa Jaramogi waonya Winnie na Junior kwa uhasama na Oburu

Na RUSHDIE OUDIA January 21st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

UHASAMA katika familia ya Jaramogi Oginga Odinga umechukua mwelekeo mpya baada ya ukoo wa Kawuor kuwashutumu wana wawili wa marehemu Raila Odinga kwa kumkosea heshima Kiongozi wa ODM Oburu Oginga.

Ukoo huo umewashutumu Winnie Odinga, Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) na Raila Junior ambao ni wanawe Raila kwa kuaibisha familia hiyo na kuanika uhasama wao hadharani.

“Kitendo cha Winnie na Raila Junior kumkosea Dkt Oburu heshima hakifai kutokea tena. Kama wazee tunaotoa wito kwa watoto wetu hawa waheshimu baba yao ambaye ni mwana wa kiume wa kwanza wa Jaramogi,” akasema William Ojwang,’ mmoja wa wazee hao. Duru zinaarifa walikuwa wamekutana na Dkt Oburu kabla ya kuafikiana kuandaa kikao hicho.

“Mlango wetu u wazi kwa mazungumzo na Nyaroche (Winnie) usimwaangalia babako na kuzungumza mabaya kumhusu. Usifanye hivyo,” akaongeza.

Wikendi, Winnie na Raila waliandaa mkutano mkubwa wa kisiasa Mtaa wa Kibra Nairobi huku Dkt Oburu na wabunge wengine wa ODM wakizuru Magharibi mwa Nchi kuvumisha chama.

Jana, wazee, watoto wa Jaramogi, wajuu wake na vitukuu waliandaa kikao Kisumu, siku ambayo pia ni miaka 32 tangu kifo cha makamu huyo wa rais wa kwanza nchini.

Ingawa walipuuza kuwa kuna mgawanyiko kwenye familia hiyo, uamuzi wa kuwakaripia Winnie na Raila Junior ulionyesha taharuki ambayo inaendelea kushuhudiwa kati ya familia ya marehemu Raila na ile ya Dkt Oburu.

Wazee wa Kawuor wakizungumza Kangó ka Jaramogi walitoa wito kwa Dkt Oburu apewe heshima yake kama kiongozi wa ODM.

Walisema Seneta huyo wa Siaya anatosha kuongoza chama baada ya kushirikiana na babake Jaramogi kisha kufanya maamuzi muhimu kisiasa akifanya kazi na Raila.

Taifa Leo ilipomfikia Raila Junior na Winnie kuhusu kauli yao, Winnie hakupatikana kwa simu naye Raila Junior akasema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa.

“Sina maoni kwa sasa,” akasema Raila Junior.

Omondi Oginga, mwanawe Jaramogi na nduguye Dkt Oburu alikanusha kuwa kuna uhasama kati yao.