Habari za Kitaifa

Mamia ya wavulana wapitwa na masomo wakikesha jandoni

Na FLORAH KOECH January 22nd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MAMIA ya wavulana wa shule katika eneo la Tiaty, Kaunti ya Baringo, bado hawajarejea shuleni zaidi ya wiki mbili tangu muhula wa kwanza ulipoanza wakiwa jandoni kutokana na tohara iliyofanyika wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

Walimu wakuu wameonya kuwa kutokuwepo kwa wanafunzi hao kwa muda mrefu kunalemaza shughuli za masomo, huku kukiwa na hofu kuwa baadhi yao huenda wasirudi kabisa shuleni, jambo linaloweza kusababisha kushuka kwa viwango vya usajili, hasa kwa wavulana wa madarasa ya juu wanaoweza kushindwa kuhimili masomo wanaporejea.

Miongoni mwa shule zilizoathirika ni Kreze, Sukut, Katagh, Ptikii, Ng’oron, Korelach, Nalekat, Donyasas, Nakoko, Lorwatum, Cheseret, Domo, Chesirimion, Riong’o, Naudo, Akwichatis na Nasorot.

Katika Shule ya Msingi ya Domo, iliyoko Kaunti-ndogo mpya ya Kolowa, wavulana 15 wa Gredi 4 hadi 9 bado hawajaripoti shuleni.

“Tunaelezwa kuwa wavulana kutoka jamii hii, wakiwemo wanaosoma, walifanyiwa tohara wakati wa sikukuu na bado wako jandoni. Zaidi ya wavulana 15 hawajarejea, na hatujui ni lini watarudi,” alisema mwalimu mkuu Charles Chesire.

Alisema kwa mujibu wa mila ya Wapokot, waliotahiriwa wanatarajiwa kutengwa kwa zaidi ya miezi mitatu.

Alihimiza mamlaka za eneo hilo kufuatilia suala hilo kwani masomo tayari yameanza.

“Tunaomba wazazi wahakikishe kuwa kama sherehe za kitamaduni ni lazima, basi zifanyike wakati wa likizo za shule ili watoto warudi masomoni shule zinapofunguliwa. Inasikitisha sana kuona watoto wakikosa masomo kwa sababu ya mila,” alisema.

Katika Shule ya Msingi ya Donyasas, Tiaty ya Kati, wavulana tisa bado hawajaripoti. Mwalimu mkuu Mathew Chesire alisema wavulana hao, wengi wao wakiwa wa madarasa ya nne hadi 10, bado wako kwenye mchakato wa tohara.

“Tunatarajia machifu wafuatilie suala hili na kuhakikisha wanafunzi wote wanahesabiwa, kwa sababu baadhi wamekuwa jandoni tangu walipofanyiwa tohara miezi miwili iliyopita,” alisema.

Shule ya Msingi ya Korelach pia ina idadi ndogo ya wanafunzi.

Kati ya zaidi ya wanafunzi 120, ni 88 pekee waliohudhuria masomo, huku wavulana 18 wakiwa bado hawajarudi kwa sababu ya tohara.

Mwalimu mkuu Cliophas Lotuliangiro alisema anapanga kuitisha mkutano na machifu, wazazi na kamati ya shule ili kushughulikia hali hiyo na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu.

“Katika maeneo haya, mila za kitamaduni bado zinazingatiwa kwa kiwango kikubwa, na kutokana na viwango vya juu vya kutojua kusoma na kuandika, kuna haja ya kuelimisha jamii kwa nini watoto lazima waende shuleni.

“Kama tohara ni lazima, basi haifai kufanyika wakati shule zimefunguliwa kwa sababu huvuruga masomo,” alisema. Aliongeza kuwa ingawa mila hiyo ni muhimu kwa jamii, lazima itambue elimu.

“Ikiwa sherehe za tohara zitafanyika wakati wa muhula, kuna hatari ya kupoteza wanafunzi kabisa,” alisema.

Mzee Yuda Losutan alieleza historia ya tohara, akisema awali sherehe hizo zilichukua miezi mitatu hadi minne na zilikuwa kwa wavulana wenye umri wa miaka 16 na zaidi.

“Mambo yamebadilika. Siku hizi hata wavulana walio chini ya miaka kumi wanatahiriwa, hali inayoathiri masomo yao kwa kuwa wanaweza kukaa jandoni kwa zaidi ya miezi mitatu,” alisema.

Hata hivyo, maafisa wa serikali wamesema wanachukua hatua kuhakikisha watoto wanarejea shuleni. Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Tiaty Kati Aaron Omaset, alisema anafanya ukaguzi wa ghafla shuleni kufuatilia wanafunzi ambao bado hawajaripoti.

“Sina idadi kamili ya wavulana walio nje ya shule, lakini ninafanya msako vijijini kuhakikisha watoto wote, wakiwemo waliotahiriwa, wanarejea shuleni,” alisema.

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Kolowa, Edward Karanja, alithibitisha kuwa vituo vyote 21 vinavyotumiwa kama jandoni vilifungwa baada ya sikukuu.

Alisema atakusanya takwimu kamili za wanafunzi shuleni wakati wa mkutano wa wadau wa elimu utakaowaleta pamoja walimu wakuu na maafisa wa mtaala.

“Hakuna mwanafunzi anayepaswa kuwa nje ya shule sasa kwa kuwa vituo vya jandoni vimefungwa,” alisema.