Mazungumzo kwenye WhatsApp na SMS ni mikataba halali kisheria, korti yapitisha
MAZUNGUMZO ya kawaida kupitia WhatsApp yanaweza kuwa mkataba wa kibiashara. Hali ni iyo hiyo kwa ujumbe mfupi wa simu (SMS).
Hilo ndilo onyo la wazi kutoka kwa Mahakama Kuu, ambayo imeamua kuwa jumbe za kidijitali zinaweza kuunda mikataba halali inayotekelezeka kisheria iwapo vipengele vya msingi vya sheria vitathibitishwa.
Uamuzi huo ulitolewa na Mahakama Kuu ya Siaya katika rufaa ya kesi iliyoanzia mahakama ya kesi ndogo kati ya Fredrick Ochiel na Kennedy Okoth, marafiki wa kibiashara ambao makubaliano yao yasiyo rasmi kuhusu mashine ya picha za matibabu yaligeuka kuwa kesi mahakamani.
Mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo na kuidhinisha uamuzi wa mahakama ya chini uliompa Bw Okoth fidia ya Sh145,000, ikisema kuwa jumbe walizobadilishana kupitia simu zilithibitisha kuwepo kwa makubaliano halali.
Kiini cha mgogoro huo kilikuwa makubaliano rahisi.
Bw Okoth alisema kuwa mnamo Septemba 2024 alikubaliana kwa maneno kumkodisha Bw Ochiel mashine yake ya picha za matibabu kwa Sh1,000 kwa siku kwa muda wa siku 145.
Bw Ochiel alipeleka mashine hiyo mjini Nairobi, akaendelea kuitumia, akalipa Sh5,000 pekee, kisha akakosa kuirejesha. Alikana kuwepo kwa ada walizokubaliana na kusema hakukuwa na mkataba wa maandishi.
Mahakama ya awali ilimpa ushindi Bw Okoth.
Katika rufaa, Mahakama Kuu iliombwa kujibu swali linalozidi kuwa muhimu katika uchumi wa kidijitali nchini Kenya: Je, mazungumzo ya WhatsApp na SMS yanaweza kuwa mkataba wa kibiashara unaowafunga wahusika?
Jaji David Kemei alijibu kwa kauli ya ndio, mradi tu masharti ya kisheria yatimizwe.
“Ni sheria kuwa makubaliano ya mdomo yaliyofanywa kwa nia njema ni halali kisheria mradi mlalamishi aweze kuyathibitisha,” alisema jaji huyo, akirejelea Kifungu cha 107 cha Sheria ya Ushahidi kuhusu mzigo wa kuthibitisha.
Mahakama ilisisitiza kuwa mikataba si lazima iwe ya maandishi ili itekelezwe.
Kilicho muhimu ni kuwepo kwa pendekezo, kukubali, malipo na uwezo wa wahusika kufanya mkataba.
Vipengele hivyo, mahakama ilisema, vinaweza kubainika kupitia mienendo na mawasiliano ya wahusika.
“Mikataba inaweza kubainishwa kutokana na mienendo ya wahusika na si lazima iwe ya maandishi,” hukumu ilisema.
Katika kesi hii, ushahidi wa kidijitali ulikuwa muhimu.
Mahakama ilichunguza jumbe za SMS na mawasiliano ya WhatsApp yaliyowasilishwa na Bw Okoth.
Jumbe hizo zilionyesha mazungumzo kuhusu ada ya kila siku, ahadi za kulipa kufikia tarehe fulani, maelezo ya kuchelewa kulipa, na maombi ya kulipa angalau asilimia 60 ya deni lililokuwa limesalia.
“Imebainika kuwa wahusika hawakutia saini mkataba wa maandishi, lakini kuna jumbe kadhaa za SMS na mawasiliano ya WhatsApp yaliyowasilishwa kama ushahidi wa makubaliano,” mahakama ilisema.
Bw Ochiel alikiri kuchukua mashine hiyo na kukubali kuwa alilipa Sh5,000, jambo ambalo “limeandikwa wazi katika mawasiliano hayo”.
Kutokana na ushahidi huo, mahakama ilisema kulikuwa na “makubaliano ya wazi ya nia.” Ilibainisha kuwa “masharti ya makubaliano ya mdomo yalinaswa katika mawasiliano ya SMS na WhatsApp [na] yaliwafunga wahusika.”
Mahakama pia ilibainisha kuwa kwa kuwa Bw Ochiel hakupinga kuwasilishwa kwa ushahidi wa mawasiliano hayo, ilichukuliwa kuwa wahusika wote waliyakubali kama ushahidi.
Bw Ochiel alikuwa amepinga kukubalika kwa jumbe hizo, akidai hazikuwa na cheti chini ya Kifungu cha 106B cha Sheria ya Ushahidi.
Mahakama ilikataa hoja hiyo, ikisema hakupinga wakati ushahidi uliwasilishwa, na hivyo alikubali mawasiliano hayo kama sehemu ya ushahidi.
Uamuzi huu unabeba funzo kubwa kwa wafanyabiashara na watu binafsi wanaofanya miamala isiyo rasmi.
Mahakama, jaji alisema, hazitaandika upya mikataba kwa sababu tu mhusika mmoja anajutia masharti aliyokubali.