IEBC yasota, yasema haina pesa za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeonya kuwa pengo la Sh13 bilioni katika bajeti ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 itaathiri pakubwa maandalizi ya tume hiyo, kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa katika Bunge la Kitaifa.
Haya yalibainika huku wabunge wakishinikiza kutekelezwa kwa Hazina ya IEBC “kama inavyotakiwa kisheria ili kuimarisha uhuru wa kifedha wa tume na kuifanya iache kutegemea utoaji wa fedha wa hiari kutoka Wizara ya Fedha.”
Stakabadhi zilizowasilishwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Hussein Marjan, kwa Kamati ya Bunge ya Utekelezaji Usimamizi wa Masuala ya Katiba (CIOC), zinaonyesha kuwa, eneo litakaloathirika zaidi na uhaba wa fedha ni malipo ya mishahara ya maafisa wa uchaguzi, ambayo yanahitaji Sh7.63 bilioni.
Tume hiyo pia imelimbikiza madeni ya takribani Sh5.75 bilioni, hasa ada za kisheria, kutokana na chaguzi zilizopita.
“Madeni haya yamekuwa yakiongezeka kwa muda na yataathiri vibaya shughuli za tume katika kuendesha Uchaguzi Mkuu wa 2027,” IEBC inasema.
Kamati ya CIOC, inayoongozwa na Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, katika ripoti yake kwa Bunge la Kitaifa, imeonya kuwa “pengo hili la kifedha linatishia uwezo wa tume kutekeleza ipasavyo wajibu wake wa kikatiba,” huku ikiitaka Wizara ya Fedha kushughulikia wasiwasi wa IEBC kuhusu upungufu wa bajeti.
“Kamati inapendekeza Wizara ya Fedha ishughulikie nakisi ya bajeti iliyoibuliwa na IEBC kwa Uchaguzi Mkuu wa 2027 na itoe ratiba wazi ya utoaji wa fedha mapema kama ilivyoombwa na tume ili kuhakikisha utekelezaji wa shughuli za uchaguzi kwa wakati,” ripoti ya CIOC inasema.
Tume hiyo pia imelalamikia ukosefu wa fedha za kulipa madeni ya kihistoria yanayohusiana na chaguzi za awali, ikionya kuwa “endapo madeni haya hayatalipwa, yataongezeka na kudhoofisha shughuli za tume,” kauli ambayo pia iliungwa mkono na CIOC.
“Tume imebaini kuwa, italazimika kushughulikia kesi nyingi mahakamani,” ripoti ya CIOC inaeleza.
Kamati hiyo iliongeza kuwa, kulipwa kwa madeni hayo “kutasaidia kurejesha imani ya wasambazaji na kuhakikisha uwezo wa kiutendaji wa tume hauathiriki.”
IEBC ina jukumu la kusimamia au kuendesha kura za maamuzi na chaguzi za nyadhifa zilizoanzishwa na Katiba, pamoja na chaguzi nyinginezo zilizofafanuliwa kisheria.
Pia, tume hiyo ina wajibu wa kudhibiti na kuweka mipaka ya maeneobunge na wadi, kusajili wapigakura na kusimamia shughuli za uchaguzi na uhamasisho wa mpigakura pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano ya uchaguzi.
Wakati wa maandalizi ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/26, IEBC iliomba Sh61.74 bilioni kwa Uchaguzi Mkuu wa 2027, fedha ambazo zingetengwa katika miaka mitatu ya kifedha: 2025/26, 2026/27 na 2027/28.
Mpango huo wa bajeti, ambapo Sh55 bilioni zingetolewa na Wizara ya Fedha, ulitumika kama msingi wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Katika mpango wake wa bajeti, tume hiyo ilipendekeza Sh15.3 bilioni zitolewe mapema katika mwaka wa kifedha wa 2025/26 ili kuwezesha shughuli za kabla ya uchaguzi, “hasa usajili wa wapigakura na ununuzi wa mifumo na vifaa vya teknolojia ya uchaguzi.”
Hata hivyo, ni Sh9.33 bilioni pekee zilizoidhinishwa na Bunge la Kitaifa, kama ilivyothibitishwa na Mdhibiti wa Bajeti (CoB), Dkt Margaret Nyakang’o, katika ripoti yake ya utekelezaji wa bajeti ya serikali ya kitaifa ya Novemba 2025 kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2025/26.
Katika mwaka wa kifedha wa 2026/27, tume imepanga bajeti ya Sh25.4 bilioni, huku ikipanga Sh21 bilioni kwa mwaka wa kifedha wa 2027/28.
Waziri wa Fedha, John Mbadi, hakujibu maswali yetu tuliyomtumia kuhusu haja ya kufadhili IEBC ipasavyo ili iweze kutekeleza wajibu wake kama inavyotakiwa kikatiba na Sheria ya IEBC.
Hata hivyo, awali Bw Mbadi amekuwa akizungumza wazi kuhusu gharama kubwa ya chaguzi nchini, huku wataalamu wa masuala ya uchaguzi wakihusisha gharama hiyo na upungufu wa imani kwa tume miongoni mwa Wakenya.
“Bajeti ya IEBC inapaswa kuwa yenye ufanisi. Tutawauliza maswali magumu ili kuhakikisha wanatumia fedha za umma kwa njia bora,” alisema Bw Mbadi katika mkutano wa awali na wabunge, akihimiza tume hiyo kuwa makini katika usimamizi wa fedha za umma.
Ununuzi wa vifaa vipya vya Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Uchaguzi wa Kenya (KIEMS) kuchukua nafasi ya vifaa 45,352 vilivyopo ambavyo vinachukuliwa kuwa vya zamani na vilivyopitwa na teknolojia, pia ni sehemu ya Sh61.74 bilioni ambazo tume inaomba kwa Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Ili kununua vifaa hivyo, IEBC inaomba Sh7.04 bilioni, pamoja na Sh2.6 bilioni zinazohitajika kuboresha na kudumisha mifumo ya uchaguzi.
Vifaa hivyo vilinunuliwa mnamo 2017 kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo, na kwa kuzingatia kanuni kwamba teknolojia hupitwa na wakati baada ya miaka 10, ina maana kuwa ili kuhakikisha uaminifu wa Uchaguzi Mkuu wa 2027, tume haina budi kununua vifaa vipya.
Hii ina maana kuwa ni vifaa 14,000 vya KIEMS vilivyonunuliwa mnamo 2022 pekee ndivyo vitakavyotumika.
Nchi inahitaji jumla ya vifaa 59,352 vya KIEMS, huku 3,959 vikitengewa mafunzo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2027.
IEBC inakadiria kusajili wapigakura wapya milioni 5.7, wengi wao wakiwa vijana watakaofikisha umri wa kupiga kura ifikapo 2027, huku ikipanga kuchapisha rasmi vituo 55,393 vya kupigia kura, kutoka vituo 46,229 vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.