Habari za Kitaifa

Mikakati ya 2027 Ruto aliyofichulia vigogo wa UDA katika mkutano usiku

Na MOSES NYAMORI, KEVIN CHERUIYOT January 22nd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ameanza kupanga kampeni za kuchaguliwa tena kuanzia mashinani kwa kuitisha mikutano miwili mikubwa; mmoja wa viongozi wote waliochaguliwa kwa tiketi ya United Democratic Alliance (UDA), na mwingine unatakaowaleta pamoja wanaowania tiketi za chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Mnamo Jumanne, Rais Ruto alipokea taarifa kutoka kwa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya chama (NEB) pamoja na Kamati ya Kutatua Migogoro ya Uchaguzi na Uteuzi (ENDRC) kuhusu uchaguzi wa mashinani uliokamilika hivi majuzi.

Ni katika mkutano huo wa Jumanne usiku ambapo Rais aliagiza kufanyika kwa uchaguzi wa marudio, kufuatia malalamiko ya viongozi waliochaguliwa kuwa hawakuhusishwa ipasavyo katika zoezi hilo.

Rais ameitisha kikao maalumu cha Baraza la Kitaifa la Uongozi (NGC) kitakachofanyika Jumatatu, Januari 26, huku mkutano mwingine na wanaowania tiketi ya UDA katika uchaguzi wa 2027 ukipangwa kufanyika Februari 4.

Hatua hii inalenga kujenga mitandao imara ya kisiasa mashinani kwa kampeni ya kumrejesha madarakani.

Kikao cha NGC kitahudhuriwa na magavana wa UDA, manaibu magavana, maseneta, wabunge wa Bunge la Kitaifa, wawakilishi wa wanawake, wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) pamoja na wawakilishi wa wadi katika mabunge ya kaunti. Mikutano yote miwili itafanyika katika Ikulu ya Nairobi.

Dkt Ruto pia ameagiza uchaguzi wa marudio mashinani katika vituo kadhaa vya kupigia kura katika kaunti 42, hatua inayolenga kuzuia migawanyiko mikubwa ndani ya chama.

Chama hicho kinapanga kuchagua jumla ya maafisa 20 katika kila kituo cha kupigia kura.

Kwa jumla, UDA inalenga kuwa na takriban maafisa 600,000 wa mashinani kote nchini, idadi ambayo chama kinasema ni muhimu katika kuimarisha mitandao thabiti ya kisiasa.