Wakenya katika TikTok walivyosaidia mwanamke kufufua biashara iliyokwama
MFANYABIASHARA wa Nakuru, Harriet Akinyi, 28, aliposambaza video halisi zikionyesha alivyokuwa akipambana kuendesha mkahawa wake wa ‘Tule Kienyeji’ jijini Nakuru kupitia TikTok, hakufikiria kuwa zingesababisha wimbi la upendo na mshikamano kote nchini.
Kilichoanza kama kilio cha kukata tamaa kutoka kwa mfanyabiashara huyo, kimedhihirisha nguvu ya mshikamano wa Wakenya katika mitandao ya kijamii.
Katika video isiyo na tarehe, iliyorekodiwa ndani ya mkahawa wake, Akinyi alionekana akilia huku akieleza changamoto za kuendesha biashara aliyofungua miezi michache iliyopita.
Alifichua kuwa licha ya kuwekeza fedha nyingi, siku zilipita bila kupata mteja hata mmoja.
Wakenya waliunda nambari ya malipo kumsaidia, huku wakazi wakimiminika mkahawani kwa siku mbili mfululizo kununua chakula, unga, mayai, mafuta ya kupikia, vinywaji na misaada ya kifedha.
Wengine walisafiri kutoka Nairobi, Nyeri, Kiambu, Meru, Kisii na Eldoret kumsaidia.
Kufikia Jumatano asubuhi, mkahawa uliokuwa mtupu ulikuwa umejaa wateja na foleni ndefu.
“Nimejaribu kwa uwezo wangu wote. Nimewekeza pesa zote nilizokuwa nazo kwa matumaini ya kupata mauzo, lakini imekuwa bure. Wateja hawaji kabisa,” alisema huku akilia, akiongeza kuwa hali hiyo ilikuwa imemfikisha pabaya.
“Kwa sasa nina Sh35 tu kwenye akaunti yangu ya benki na Sh4 taslimu,” alisema.
Akinyi alieleza kuwa alifungua mkahawa wake kando ya Barabara ya Maasai, karibu na Hospitali ya Mercy Mission, akitumaini eneo hilo, kilomita chache kutoka katikati ya jiji, lingevutia wateja. Alitumia takriban Sh150,000 kutoka kwa akiba yake na msaada wa marafiki ili kuanzisha biashara hiyo.
Badala yake, alikumbana na viti vitupu, hasara kuongezeka na chakula kuharibika, hali iliyomsukuma kufikia mojawapo ya nyakati ngumu zaidi maishani mwake.
Uaminifu wake katika kueleza changamoto hizo uligusa wengi. Wakenya waliunda nambari ya malipo kumsaidia, huku wakazi wakimiminika mkahawani kwa siku mbili mfululizo kununua chakula, unga, mayai, mafuta ya kupikia, vinywaji na misaada ya kifedha.
Wengine walisafiri kutoka Nairobi, Nyeri, Kiambu, Meru, Kisii na Eldoret kumsaidia. Kufikia Jumatano asubuhi, mkahawa uliokuwa mtupu ulikuwa umejaa wateja na foleni ndefu.
Akinyi alisema alizidiwa na wema huo.
“Nimeguswa sana. Sikutarajia video ile ivume kiasi hiki. Niliirekodi kama kilio cha dhati cha kuomba msaada. Nawashukuru sana Wakenya,” alisema.