Afya na Jamii

Utafiti wahofia glakoma itachangia upofu wa mamilioni kufikia 2060

Na WANGU KANURI January 22nd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

UTAFITI uliofanywa na Taasisi ya Ophthalmology, Uingereza, unaonyesha kuwa kufikia mwaka wa 2060, zaidi ya watu milioni 1.6 wenye umri wa miaka 40 na kuendelea wanaweza kuathiriwa na ugonjwa wa glakoma.

Glakoma hutokea pale ambapo presha inapojikusanya ndani ya jicho, na kuharibu neva ya macho inayobeba ishara za kuona kwenda kwenye ubongo.

Hali hii inaweza kusababisha kupungua kwa uwezo wa kuona na hata upofu.

Glakoma huonekana zaidi kwa watu wenye umri wa miaka 50 na zaidi, lakini mara nyingi haina dalili hadi mwisho, ambapo upotevu wa uwezo wa kuona huwa tayari ni wa kudumu.

Aina ya glakoma inayoharibu neva ya ndani ya jicho kwa kuziba mfumo wa utoaji maji hivyo kusababisha presha inayoharibu neva, ndiyo huwaathiri watu wengi.

Mara nyingi hakuna dalili za awali, ndiyo maana angalau asilimia 50 ya watu wenye glakoma hii hawajui wanaugua.

Kwa sasa, glakoma haina tiba, lakini ikigundulika mapema, mtu anaweza kulinda uwezo wake wa kuona na kuzuia hali ya kutoona.

Mtu yeyote anaweza kupata glakoma, lakini watu weusi wenye umri wa zaidi ya miaka 40, watu wote wenye umri wa zaidi ya miaka 60, wenye historia ya glakoma kwenye familia na wanaougua ugonjwa wa kisukari wapo kwenye hatari zaidi.