Afya na Jamii

Sababu ya vidonda ndugu kutosikia matibabu kabisa

Na PAULINE ONGAJI January 23rd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

JE, umewahi kujiuliza kwa nini baadhi ya vidonda sugu huendelea kwa miezi au hata miaka bila kupona, licha ya kupata matibabu?

Utafiti mpya unaonyesha kuwa jibu huenda halihusiani sana na kushindwa kwa viuavijasumu kama ilivyodhaniwa awali, bali ni njama fiche ya kibayolojia inayosukwa na bakteria wa kawaida.

Utafiti huo unaonyesha kuwa bakteria wanaopatikana kwenye vidonda hivi hutekeleza jukumu zaidi ya kupinga dawa; huachilia sumu zinazoshambulia, kuzidi nguvu na kupooza seli za ngozi zinazohusika na ukarabati wa jeraha, hivyo kusimamisha kabisa mchakato wa kupona.

Muhimu zaidi, utafiti huo unaelekeza wataalamu kwenye suluhisho lenye matumaini: kuzima uzalishaji wa sumu hizi huruhusu seli za ngozi kupona na kurejelea kazi yao ya asili ya kuponya jeraha.

Matokeo hayo, yaliyochapishwa katika jarida la Science Advances, yametolewa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nanyang, Singapore (NTU Singapore) na Chuo Kikuu cha Geneva.

Yanatoa matumaini mapya katika matibabu ya vidonda ndugu, vikiwemo vile vilivyoambukizwa bakteria sugu kwa viuavijasumu.

Vidonda ndugu ni tatizo kubwa la kiafya duniani. Kila mwaka, takribani watu milioni 18.6 ulimwenguni hupata vidonda vya mguu kutokana na kisukari, aina kuu ya vidonda sugu ambapo, hadi mtu mmoja kati ya watatu wenye kisukari huathirika.

Vidonda hivi ni sababu kuu ya kukatwa kwa viungo vya chini vya mwili, na huwanasa wagonjwa katika mzunguko wa maambukizi yasiyoisha, kupona kwa kuchelewa na kulazwa hospitalini mara kwa mara.

Utafiti ulilenga ‘mhusika’ mkuu anayepatikana mara nyingi kwenye vidonda hivi sugu: bakteria aina ya Enterococcus faecalis.

Bakteria huyu hutumia fursa kusababisha maambukizi ya muda mrefu katika vidonda vya mguu kutokana na kisukari, na kuongezeka kwa aina zinazopinga viuavijasumu kumeifanya tiba kuwa changamoto zaidi.

Ingawa madaktari wamekuwa wakijua kwa muda mrefu kuwa maambukizi huzuia kupona, utaratibu halisi wa kisayansi ulikuwa haujaeleweka.

Wanasayansi waligundua kuwa E. faecalis huingilia mchakato wa kupona kwa njia tofauti na bakteria wengi wa vidonda.

Badala ya kutegemea sumu pekee, bakteria huyu huachilia kemikali hatari ambazo huharibu seli za binadamu na kuvuruga ukarabati wa kawaida wa tishu.

E. faecalis huzalisha kemikali kwa mfululizo inayosababisha msongo mkali katika tishu za jeraha.

Mlipuko wa kemikali hii huzidi uwezo wa seli za ngozi zinazofunga jeraha. Majaribio ya maabara yalionyesha kuwa msongo huo huzima seli zinazosaidia kupona.

Ili kuthibitisha uhusiano huo, watafiti walijaribu aina ya E. faecalis iliyobadilishwa kijenetiki. Bakteria hao walizalisha kiwango kidogo sana cha kemikali na hawakuzuia tena kupona kwa jeraha.

Muhimu zaidi, watafiti waligundua kuwa seli za ngozi zilizokuwa zimepata msongo ziliweza tena kukua na kurekebisha jeraha baada ya msongo kudhibitiwa.

“Matokeo yetu yanaonyesha kuwa badala ya kujaribu kuua bakteria kwa viuavijasumu pekee, tunaweza kuzuia bidhaa hatari wanazozalisha na kurejesha mchakato wa kupona.”

Watafiti wanasema mbinu hii inaweza kubadilisha kabisa matibabu ya vidonda sugu. Tiba za baadaye zinaweza kujumuisha bandeji zinazolinda seli za ngozi na kuchochea kupona, hata pale bakteria sugu kwa dawa wanapokuwepo.

Watafiti wanaamini mkakati huu unaweza kuhamishwa kutoka maabara hadi hospitali kwa kasi zaidi kuliko ukuzaji wa viuavijasumu vipya.

Kikosi cha utafiti sasa kinapanga kuelekea kwenye majaribio ya kitabibu kwa binadamu huku kikiendelea na tafiti kwa wanyama ili kuboresha mbinu za matibabu ya vidonda sugu.